Washiriki wa Kisura wa Tanzania 2009 walishiriki katika warsha fupi mwisho wa wiki iliyopita ikiwa kama sehemu ya mafunzo yao wakiwa kambini.
Warsha hiyo iliyofanyika katika Hoteli ya Kiromo mjini Bagamoyo ilikuwa na lengo la kuwapatia visura hao elimu ya usimamizi wa fedha na ustaarabu yaani ‘etiquette.’
Akizungumzia warsha hiyo Meneja Mradi wa Kisura wa Tanzania 2009 Grace Kilembe alisema kuwa warsha hiyo ni sehemu ya mafunzo kwa wasichana hao wakiwa kambini.
“Moja ya malengo ya Kisura wa Tanzania ili aweze kujitambua, ni kuwapatia elimu ili waweze kutambua umuhimu wao katika jamii, uwezo walionao na mambo wanayoweza kutenda katika jamii na katika maisha yao kwa ujumla. Hivyo basi warsha hii ni muhimu sana kwao kwa sababu inawapa ujuzi wa usimamizi wa fedha na ustaarabu katika mazingira tofauti,” alielezea Grace.
Katika masuala ya ustaarabu wasichana hao walifunzwa jinsi kusalimiana, adabu za mezani, ustaarabu wa simu, kuwahi, matumizi na usafi binafsi. Somo hili lilitolewa na Sarah Majengo kutoka kampuni ya Innovative Creations.
Katika somo lake Sarah aliwaeleza wasichana umuhimu wa usafi kwa ujumla, jinsi ya kujitambua, na kuweza kujitokeza kisahihi kwatika mzingira tofauti.
“Kama mrembo lazima ujue jinsi ya kujimudu katika mazingira tofauti. Ni muhimu ufahamu ustaarabu wa mazingira unayokuwepo kama vile sehemu za sala, ofisi au starehe. Hii inajumuisha mavazi na jinsi ya kusalimia katika mazingira haya,” aliongeza Sarah.
Kuhusu usimamizi wa fedha Bi Chaba Mavura Meneja Mkuu wa kampuni ya Eazy Finance alitoa elimu ya usimamizi wa fedha.
“Ni Muhimu sana kujua jinsi ya kupanga matumizi yako ukiwa unatoa kipaumbele mahitaji ambayo ni ya muhimu kwa binadamu kama vile malazi, chakula na afya kabla ya kutumia pesa kwenye vitu vya anasa kama urembo na starehe. Mkiwa kwenye shindano kama hili mmoja wenu lazima ataibuka mshindi wa pesa na hivyo basi inapasa kujua jinsi ya kutumia pesa kwa uangalifu na vile vile kuwekeza ili kuongeza kipato chako,” alisema Chaba.
Washiriki wote walishiriki ipasavyo katika warsha hiyo fupi wakionekana kufurahia elimu waliyokuwa wakipata na kuuliza maswali mengi kuhusu masuala ya fedha na ustaarabu. Baada ya somo la usimamizi wa fedha visura hao walipewa zoezi dogo la kila mtu kuandika jinsi atakavyotumia shilingi 50,000 na mshindi wa shindano hilo kisura Ressoni Soto alijinyakulia kitita hicho cha elfu hamsini.
Visura wakiwa kambini hapo hupata mafunzo mbali mbali na hadi sasa wameshapata elimu ya ukimwi kupitia FHI, vile vile masuala ya kijamii na kilimo.
Shindano la kisura kwa mwaka huu linalodhaminiwa na Kampuni ya Bia ya Serengeti litafikia tamati tarehe 18 Desemba ambapo mshindi atatangazwa katika hoteli ya Movenpick jijini Dar Es Salaam.
Wadhamini wengine wa shindano hilo ni Kiromo View Hotel, Family Health International (FHI), Air Tanzania, Mwananchi Communication, EM entertainment, Clouds fm, Hugo Doming na Mercy G Beauty Parlour.