Benjamin Sawe Maelezo Dar es Salaam.
Msajili wa Vyama vya Siasa John Tendwa ameliasa Baraza la Vyama vya Siasa kuhakikisha uchaguzi wa mwaka huu unakuwa wa Kidemokrasia na wa amani.
Bwana Tendwa alisema hayo jana (leo) jijini Dar es Salaam wakati akifungua mkutano wa kwanza wa Baraza la vyama vya siasa ambapo alilitaka Baraza lililoundwa kisheria kuishauri serikali na jamii hasa katika kipindi cha uchaguzi.
Aidha alisema Baraza hilo si la kujitolea bali limeundwa kwa mujibu wa sheria na linawajibika kwa serikali na ni mshairi mkuu wa serikali katika shughuli za kisiasa. Alisema ni wajibu kwa baraza hilo kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani na utulivu na alilitaka baraza hilo kutoa tamko kulaani vitendo vinavyovunja amani na sheria ikiwa ni pamoja na kukemea vyama vya siasa vilivyoanza kampeni kabla ya tarehe ya kampeni.
Pia alivionya vyama vya siasa kuachana na siasa za kutumia lugha ya matusi wakati wa kampeni na ni wajibu wa Baraza hilo kutoa miongozo mbalimbali ambayo itafuatwa na vyama vya siasa.. Bwana Tendwa alilitaka Baraza hilo kuitisha mikutano ya mara kwa mara ambapo itatoa miongozo ambayo italiweka taifa katika mahala pazuri ili kufanikisha uchaguzi kwa amani na utulivu.
Alisema baadhi ya vyama vya siasa vimeanza kapeni kabla ya uchaguzi na vinajua kufanya hivyo ni kukiuka sheria za uchaguzi na moja ya athari za kuanza kampeni kabla ya uchaguzi ni kuwekeana pingamizi na kama likikubalika chama kitakuwa hakina mgombea hivyo amevitaka vyama kufuata taratibu na sheria za uchaguzi.
Akitoa shukrani kwa niaba ya Baraza hilo Mwenyekiti wa Baraza hilo Dr.Emanuel Makaidi amesema hawatamuogopa mwanasiasa au chama chochote cha siasa kitakachokiuka maadili kwani Baraza hilo limeundwa kwa mujibu wa kanuni na sheria. Dr. Makaidi alisema Baraza hilo litakuwa mshauri mzuri wa Serikali katika mambo ya kisiasa hasa katika kipindi cha uchaguzi.
0 comments:
Post a Comment