Na Hillary Shoo,Iramba.
MAHAKAMA ya wilaya ya Iramba mkoani Singida imemhukumu mchungaji mmoja wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) dayosisi ya Kati adhabu ya kutumikia kifungo cha miaka 30 jela na kuchapwa vikopo 12 baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka msichana mwenye umri wa miaka 19 (jina tunalihifadhi).
Mchungaji aliyekumbwa na adhabu hiyo ya kifungo gerezani ametajwa kuwa ni Japhet Nakomolwa Kidindima (37) wa KKKT-Usharika wa Igengu wilayani Iramba.
Mapema mwendesha mashitaka mrakibu msaidizi wa polisi (ASP) Adamu Chasama alidai kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo Novemba 16, mwaka jana majira ya saa 2 usiku kwenye korongo moja.
Mbele ya hakimu mkuu mfawidhi wa mahakama hiyo, Mrisho Kariho ilidaiwa kuwa siku moja kabla ya tukio hilo la ubakaji, mchungaji huyo alikwenda nyumbani kwa mwanamke mmoja wa waumini wake na kumwomba amtafutie wasichana wawili kwa ajili ya kuwapeleka kwa kaka yake jijini Dar-es-Salaamu siku inayofuata kufanyakazi za ndani.
Aidha ilielezwa kuwa baada ya kupata wasichana hao muumini huyo aliwapeleka wote kwa mchungaji majira ya jioni lakini akachagua mmoja mwenye miaka 19 na kumwacha wa 18 kwa madai kuwa kaka yake amempigia tena simu akitaka mmoja tu.
Ilidaiwa kuwa baada ya muumini huyo na binti aliyeachwa kuondoka kurejea nyumbani, mchungaji huyo alimpakia kwenye baiskeli msichana aliyemchagua na kuanza safari ya kwenda kijiji jirani cha Ibaga kwa ajili ya kupanda basi kwenda Dar-esalamu kesho yake.
Hata hivyo ilielezwa kuwa walipofika njiani kwenye korongo moja mchungaji huyo alianza kumtomasa-tosa msichana huyo kisha kumbaka kabla ya kwenda kumtelekeza ndani ya basi. Ilielezwa kuwa msichana huyo alilala ndani ya basi kabla ya kuchukuliwa na wasamaria wema kesho yake baada ya kuteremshwa kutokana na kukosa nauli, hali iliyosabisha kupelekwa kituo cha polisi na baadaye hospitalini kwa uchuguzi kisha mchungaji kukamatwa.
Akisoma hukumu hakimu Kariho alisema kutokana na ushahidi wa mazingira kuthibitisha kosa pasipo kuacha shaka lolote mchungaji huyo atatumikia kifungo cha miaka 30 jela na kuchapwa viboko 12 ili iwe fundisho kwa wengine wenye nia ya kutenda kosa kama hilo.
"Wewe nilitegemea kwa kuwa ni mchungaji unayefundisha watu maadili mema sitegemei kama unaweza kufanya kitendo cha aibu namna hii hivyo, hivyo sina sababu ni kwa nini usitumikie kifungo hicho, utachapwa viboko 6 wakati ukiingia gerezani na vingine 6 wakati ukitoka,." alisema hakimu huyo huku akimkazia macho mchungaji huyo.
0 comments:
Post a Comment