TAMISEMI YASISITIZA HALMASHAURI ZA MIJI ZIFUNGE MIFUMO YA KOMPYUTA!


Benjamin Sawe Maelezo Dar es Salaam
Halmashauri za Miji na Manispaa nchini zimeagizwa kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2011 ziwe tayari zinatumia mfumo wa kompyuta wa Epicor katika shughuli zote wanazozifanya ili kuboresha utendaji wao wa kazi.
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ndugu Eliakimu Maswi amesema mfumo huo utaziwezesha halmashauri kuwa na ufanisi katika kudhibiti mapato na matumizi ya fedha inazozikusanya.
Ndugu Maswi alisema nia ya Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ni kuhakikisha kuwa masuala ya matumizi ya fedha katika serikali za mitaa yanaboreshwa.
Wakiwasilisha taarifa zilizopatikana baada ya kufanya tathmini katika halmashauri zilizotembelewa, Wadau wa maendeleo walisema bado halmashauri nyingi nchini hazitumii mfumo wa Epicor katika shughuli zake za ukusanyaji na matumizi ya mapato.
Ndugu Maswi alisema Mpaka mwezi Februari mwaka 2010 halmashauri zipatazo 86 zilikuwa zimewekewa mfumo huu na inatarajiwa kuwa ifikapo Juni 2010 mfumo huu utasimikwa katika halmashauri zote 133 zilizopo nchini.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Pwani Hajati Fatuma Mrisho alisema angependa ufungaji wa mfumo huo wa Epicor uanzie katika mkoa wa Pwani ili uwawezeshe watendaji katika halmashauri kumudu vema kazi zao.
Pia Mkurugenzi wa Idara ya Mifumo ya Kimenejimenti Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Ndugu Rodrick Kiwelu ambaye alikuwa mjumbe katika kikao hicho cha tathmini alisema wanatarajia ifikapo juni mwaka huu Halmashauri 47 ambazo hazijafungwa mfumo huo zitakuwa zimewekewa mfumo huo.
Epicor ni mfumo wa Kompyuta ambao ukifungwa katika halmashauri utazisaidia katika kuratibu ukusanyaji na matumizi ya mapato kwa halmashauri, kuandaa taarifa za kifedha, kufanya malipo mbalimbali kwa usahihi na utawezesha udhibiti wa matumizi holela ya fedha katika halmashauri.
Agizo hilo lilitolewa katika mkutano wa tathmini wa shughuli za maendeleo unaofanyika marambili kwa mwaka kwa lengo la kukagua miradi ya maendeleo na utendaji kazi katika halmashauri kuhusiana na matumizi ya raslimali.

You liked this post? Subscribe via RSS feed and get daily updates.

0 comments:

Post a Comment