SEKTA YA HABARI YAONESHA MAFANIKIO MAKUBWA KUFIKIA ULINGO WA BEIJING!!


Na Asteria Muhozya, Tabora

Uwiano wa Kijinsia katika fani ya habari umeonesha mafanikio makubwa ya kufikia moja ya malengo 12 yaliyobainishwa katika vipaumbele vya Ulingo wa Beijing kufuatia mkutano uliofanyika nchini China miaka 15 iliyopita.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto, Mhe. Margaret Sitta wakati akizungumza na wandishi wa habari katika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa mjini Tabora leo.
Ameongeza kuwa, azimio na Ulingo wa Beijing ni matokeo ya Mkutano wa wanawake uliofanyika Mexico mwaka 1975. Mkutano huo pamoja na mambo mengine ulitangaza Muongo wa Kimataifa wa Wanawake ambao ulibainisha maeneo makuu matatu ambayo ni kuwepo kwa uswa wa Kijinsia na kuzuia ubaguzi wa kijinsia, Ushirkikshwaji wa wanawake katika mipango ya maendeleo na mchango wa wanawake katika kuimarisha amani duniani.
Aidha, ameeleza kuwa, Tanzania ambayo ni mwanachama wa Umoja wa Mataifa imeandaa taarifa ya utekelezaji wa Ulingo wa Beijing katika kipindi cha miaka 15. Ameongeza kuwa, taarifa hiyo imebeinisha mafanikio yaliyopatikana, changamoto zilizojitokeza na mikakati ya kukabiliana na changamoto hizo.
Akirejea kongamano lililofanyika tarehe 4 Machi, 2010 mjini Tabora katika ukumbi wa Veta na kuhudhuriwa na washiriki kutoka Taasisi za Serikali, Mashirka Yasiyo ya Kiserikali, Mashirika ya Kijamii, Vyama mbalimbali vya Siasa na Mashirika ya dini, amesema kuwa, washiriki waliweza kujadili mafanikio yaliyopatikana na, changamoto zilizopo na kuweka mikakati ya utatuzi wa changamoto hizo.
Halikadhalika, Mhe. Waziri amesema kwamba, kilele cha maadhimisho yanayofanyika kesho katika uwanja wa Ali Hassan mwinyi , yana madhumuni ya kupima utekelezaji wa maazimio, matamko na mikataba mbalimbali ya Kimataifa pamoja na azimio la Umoja wa Mataifa Na.1325 kuhusu amani, wanawake na malengo ya millennia 2000.
Vilevile amesema kwamba, maadhimisho haya yatatumika pia kuwahamasisha wanawake wenye sifa za uongozi kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi wa mwaka huu 2010 pamoja na kuwahimiza kujitokeza kuchagua viongozi bora.
Kuhusu kaulimbiu ya maadhimisho, ameleeza kuwa, kila mwaka Umoja wa Mataifa huwa unaandaa kaulimbiu ya Kimataifa. Hata hivyo, nchi wanachama huitafsiri kaulimbiu hiyo katika mazingira yao kwa kuzingatia vipaumbele vya nchi husika.
Ameilezea kaulimbiu ya Siku ya Wanawake Duniani, 2010 kuwa ni ‘’ Miaka 15 baada ya Beijing: Wanawake Wanaweza, wapewe nafasi’’. Ameongza kuwa, kaulimbiu hii imezingati kuwa, mwaka 2010 ni mwaka wa 15 baada ya Mkutano Mkuu wa Wanawake uliofanyika mwaka 1995 Beijing, China. Aidha,kaulimbiu hii imezingatia kuwa huu ni mwaka wa uchaguzi Mkuu wa hapa nchini na wanawake wanao uwezo wa kuwawezesha kushika nafasi mbalimbali za uongozi, hivyo kuwaomba kuendelea kuwaamini ili wapewe nafasi hizo watakazogombea.

You liked this post? Subscribe via RSS feed and get daily updates.

0 comments:

Post a Comment