MAAFISA USTAWI WA JAMII WATAKIWA KUJIENDELEZA KIELIMU!!


Benjamin Sawe Maelezo Dar es Salaam

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii Blandina Nyoni amewaasa Maafisa Ustawi wa Jamii kutumia fursa zilizopo ili kujiendeleza na kuongeza ufanisi wa kazi katika kukabiliana na changamoto zinazohusiana na utoaji wa huduma za kiustawi wa Jamii.Rai hiyo imetolewa na Kamishna wa Ustawi wa Jamii nchini Bwana Danford Makala kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Ustawi wa Jamii Bibi Blandina Nyoni katika maadhimisho ya siku ya ya Maafisa Ustawi wa Jamii duniani.
Bi Nyoni alisema Serikali inakusudia kupanua utoaji wa mafunzo katika vituo vya Ustawi wa Jamii ikiwa ni pamoja na kuimarisha Vyuo vya Kisangara (Kilimanjaro) na Ilonga kilichopo Morogoro ili viweze kutoa watumishi wa Ustawi wa Jamii ngazi ya Cheti.
Pia Bi Nyoni alisema licha ya Serikali kuridhia mikataba ya Kimataifa ya utoaji wa huduma za Ustawi wa Jamii,Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii iko katika hatua za mwisho za kukamilisha Sera ya Taifa ya Ustawi wa Jamii ili kutokuwa na kikwazo katika haki za binadamu.Aidha amekishauri Chama cha Maafisa Ustawi wa Jamii Nchini (TASWA) kishirikiane na Mamlaka husika ili kulinda misingi na kanuni za kitaalamu katika taaluma ya Ustawi wa Jamii nchini.Awali Makamu Mwenyekiti wa TASWA Bi Zena Mabere alisema siku ya Maafisa Ustawi wa Jamii Duniani inatoa fursa kwa wataalamu wa Ustawi wa Jamii kukutana ili kujadili na kubadilishana uzoefu kuhusu utoaji wa huduma endelevu kwa jamii.

Alifafanua kuwa maadhimisho hayo yanalenga kuinua ufahamu wa jamii kuhusu mchango wa wataalamu wa Ustawi wa Jamii katika kulinda na kutetea haki za makundi maalumu katika jamii ili kuboresha maendeleo na Ustawi miongoni mwa jamii.Maadhimisho ya Siku ya Maafisa Ustawi wa Jamii Duniani hufanyika kila jumanne ya tatu ya mwezi wa tatu kila mwaka ambapo kitaifa yamefanyika Jijini Dar es Salaam na kauli mbiu ni huduma bora za kiustawi wa Jamii zinachochea maendeleo ya haki binadamu kuwa halisi.

You liked this post? Subscribe via RSS feed and get daily updates.

0 comments:

Post a Comment