HUU NDIYO UJUMBE WA ZITTO KABWE KWA WATANZANIA KUTOKANA NA KIFO CHA MZEE WETU RASHID MFAUME KAWAWA (SIMBA WA VITA)

Mh. Zitto Kabwe.
Leo tukiwa katika siku ya mwisho ya mwaka 2009 na tukijiandaa kuingia mwaka mpya wa 2010, tumepatwa na habari za msiba wa Kiongozi mwanzilishi wa Taifa letu Simba wa Vita Mzee Rashidi Mfaume Kawawa. Kwa Mtanzania yeyote kifo hiki ni pigo kubwa sana, lakini pia ni fursa ya kukumbuka vyema historia ya Tanganyika na Tanzania. Ni fursa ya kuona Watanzania waliojitoa kuona kuwa kunakuwa na Taifa kutoka miongoni mwa nchi iliyokuwa ni mkusanyo tu wa makabila zaidi ya 120. Watu waliojitoa bila kuwa na uzoefu wowote wa si tu kuongoza serikali bali muhimu zaidi uzoefu wa kukusanya makabila, dini na wasio na dini na kuunda Taifa moja imara na la kujivunia linaloitwa Tanzania. Mzee Rashidi Mfaume Kawawa ni mmoja wa watu hawa waliorithi kutoka kwa mkoloni mwingireza nchi iliyokuwa na wakazi takribani milioni 8, isiyo na chuo kikuu hata kimoja, yenye madaktari wawili tu na isiyo na mfumo kabisa. Uhai wa mzee Kawawa, kuwepo kwake na kupumua kulitupa ahueni kuwa tunapo pa kukimbilia na kujifunza kama lolote lingetokea.
Mzee Kawawa ni mfano wa kuigwa kuhusu maana halisi ya utumishi wa Umma. Alikuwa jemedari wa kutegemewa katika utekelezaji wa Dira na ajenda za kujenga Taifa bila kujali maumivu yake kisiasa. Sisi vijana tuliozaliwa miaka ya sabini mwishoni mpaka themanini hatukuona kwa jicho la kuelewa kipindi kigumu cha ujenzi wa Taifa na ujenzi wa Ujamaa nchini. Hata hivyo tulikuwa tukisikia wakubwa wakizungumza na kummlaumu sana Mzee Kawawa kutokana na utekelezaji wa sera mbalimbali kana kwamba zilikuwa ni zake na sio maamuzi ya vikao vya TANU na Serikali iliyokuwa inaongozwa na TANU. Tukiwa masomoni tumejifunza kuwa yeye ndiye alikuwa mtekelezaji mkuu wa maamuzi magumu chini ya Mwalimu Nyerere. Katika kutekeleza huku alibeba lawama za kisiasa, hakujali. Hakutikisika. Muhimu zaidi alimkinga Mwalimu Nyerere kwa yeye kubeba lawama zote za utekelezaji wa maamuzi yote ya chama. Aliweka Taifa mbele ya maslahi yake ya kisiasa. Simba wa Vita alichukulia uongozi katika mantiki ya utumishi haswa na sio katika mantiki ya sasa ya uheshimiwa. Hili ni jambo kubwa la kujifunza.
Maisha ya Mzee Kawawa Kisiasa na Kiuongozi yanawakilisha taathira ya Utanzania kwa maana ya Utu na Usawa bila ya kutumia madaraka yake kujikweza kitabaka. Watoto wa Mzee Kawawa wamesoma katika shule ambazo watoto wa Watanzania wengine wamesoma. Mimi binafsi nimesoma na binti yake anayeitwa Zainab na tulikuwa naye katika harakati za wanafunzi pale Mlimani kama mwanafunzi mwingine yeyote. Hii iliwezekana tu kwa sababu waasisi hawa wa Taifa walihakikisha kuwa shule za Umma ni bora kuweza kuelimisha Watanzania. Hivi sasa hali ni tofauti kwani viongozi tunashindana aina za shule ambazo watoto wetu wanasoma. Hii ni kwa sababu tumedidimiza shule za Umma, na kwa kuwa hazituumi ni rahisi sana kuzipuuza. Sera za kiliberali zimefanya elimu kuwa bidhaa inayouzwa katika soko. Wasisi wa Taifa hawakutaka hili kwani kama wangekuwa na fikra hizi toka mwanzoni mwa uhuru watoto wengi wa masikini ambao ndio viongozi wetu leo wasingepata elimu. Utekelezaji wa Azimio la Arusha ambalo lilitekelezwa kwa ujasiri mkubwa na Mzee Kawawa ulifungua fursa kwa watoto wote wa Tanzania bila kujali hali za wazazi wao kupata elimu na huduma nyingine za jamii. Hali ni tofauti kabisa katika nchi nyingine za Kiafrika ambapo mwenye mali ndio anapata huduma bora.
Kifo cha Mzee Kawawa ni fursa. Ni fursa ya kutafakari na kujadiliana kuhusu misingi na Dira ya Taifa letu kama ambavyo walifikiri na kuijenga wakati walipokuwa wakipigania uhuru na hata baada ya kupata Uhuru. Ni jukumu la Vijana wa sasa kuona kuwa Wazee hawa waasisi ambao ndio wanakwisha hivyo na kutangulia mbele ya haki walifanya wajibu wao - kuleta Uhuru na kujenga Taifa. Vijana wanapaswa kuhakikisha kuwa tunahodhi jukumu la kuirejesha, kuilinda na kuienzi misingi ya Taifa ya Umoja, Utu na Uzalendo kwa Taifa.
Historia inatuambia kitu kimoja kuhusu Mzee Rashidi Mfaume Kawawa. Kwamba, Kama Mwalimu Nyerere alikuwa Wino ulioandika TANZANIA, Mzee Kawawa alikuwa Kalamu. Nenda Simba wa Vita, msalimu rafikiyo kipenzi Mwalimu.

You liked this post? Subscribe via RSS feed and get daily updates.

0 comments:

Post a Comment