Kigoma waanzisha daftari la mkulima ili kupata takwimu sahihi katika Kilimo!!

Mama Salma kikwete.

Na Anna Nkinda - Maelezo, Kigoma
Serikali mkoani Kigoma imeanzisha Daftari la Mkulima litakalowezesha kupata takwimu sahihi na kupima mafanikio katika mapinduzi ya kijani ili kuratibu utekelezaji wa mapinduzi ya kilimo na kauli mbiu ya kilimo kwanza.
Hayo yamesemwa jana na Mkuu wa Mkoa huo Kanali Mstaafu Joseph Simbakalia wakati akisoma taarifa ya Maendelezo ya Mkoa kwa Mke wa Rais Mama Salma Kikwete aliyeko ziara ya kikazi ya siku mbili katika mkoa wa Kigoma. Kanali Mstaafu Simbakali alisema kuwa Halmashauri zote tatu za mkoa huo zimeshaanzisha daftari hilo ambalo limesaidia kupata "Database" ya wakulima ambayo inatoa taarifa zote muhimu za kilimo ikiwa ni pamoja na idadi na orodha ya wakulima, hekta zilizolimwa kwa kila zao, kiasi cha pembejeo kilichotumika na mavuno yanayotarajiwa kuvunwa. "Daftari la mkulima litakuwa likiboreshwa kila msimu na kimsingi takwimu zitakaopatikana katika msimu husika zitasaidia kupanga msimu unaofuata" , alisema.
Katika kuhakikisha kuwa mkoa huo unazalisha chakula cha kutosha Halmashauri zote tatu za mkoa huo zimejiwekea malengo ya kuzalisha mazao makuu manne ya chakula ambayo ni mahindi, maharage, mpunga na muhogo.
Aliendelea kusema kuwa malengo mengine ni kupanua maeneo yanayolimwa kutoka Hekta 411,810 msimu wa 2008/2009 hadi Hekta 434,950 msimu wa 2009/2010, kuongeza tija katika kilimo na kuimarisha kilimo cha umwagiliaji. Aidha uzalishaji wa mazao hayo makuu ya chakula unatarajiwa kuongezwa kutoka tani 737,270 msimu 2008/2009 hadi tani 910,316 msimu 2009/2010 sawa na ongezeko la asilimia 23.

You liked this post? Subscribe via RSS feed and get daily updates.

0 comments:

Post a Comment