wanawake walio wengi wanachangia kwa kiasi kikubwa kuharibika kwa tabia za watoto!!

Watoto wa mitaani wakiomba msaada kwa mpita njia, kumekuwa na tatizo kubwa la watoto wa mitaani ambapo moja ya mambo ambayo yamekuwa yakisababisha kuongezeka kwa watoto hao ni matatizo ya kifamilia yanayosababisha watoto kusambaratika na kwenda mitaani.
Na Anna Nkinda - Maelezo
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete amesema kuwa wanawake walio wengi wanachangia kwa kiasi kikubwa kuharibika kwa tabia za watoto wao hii ni kutokana na tabia ya kutokuwakemea pale wanapokosea na kujifanya kuwa wanakwenda na awakati.
Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) aliyasema hayo jana wakati akiongea na wanawake wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) wa mkoa wa Kagera katika ukumbi wa Lina’s Pub.
"Mnachotakiwa kukifanya ni kusimamia maadili ya watoto wenu kwani watoto wengi wanajifanya kwenda na wakati kwa kuvaa mavazi ambayo yanaacha wazi sehemu za miili yao huku wazazi wao wanafurahia huko si kwenda na wakati bali ni kupotea kimaadili", alisema
Mama Kikwete alisema, "Ni wajibu wetu kutumia fursa zilizopo kujikwamua kiuchumi na hivyo kutoa mchango wetu katika jamii na taifa kwa ujumla. Vikundi vya kiuchumi kama vile SACCOS na benki za jamii yaani VICOBA ni moja ya mikakati ambayo inatekelezwa kiutaifa ili kumkomboa kwanamke".
Akisoma taarifa ya umoja huo Kaimu katibu wa Mkoa Editha Mwinula alisema kuwa umoja huo umefanikiwa kuwahamasisha wanawake kuanzisha vyama vya Akiba na Kukopa (SACCOS) na vikundi vya uzalishaji mali ili kupunguza umaskini. Pia wanawahamasisha wanawake ili waweze kujiamini na kugombea nafasi za uongozi ili wapate kuingia katika nafasi za maamuzi ndani ya chama na serikali.
"Umoja wetu unakabiliwa na tatizo kubwa la usafiri kwani tunatumia usafiri wa baiskeli kwenye wilaya zetu lakini jiografia ya mkoa wetu ni ngumu, baiskeli haikidhi mahitaji ya watendaji ukizingatia ni kina mama. Hivyo tunashindwa kuwafikia walengwa kwa muda muafaka", alisema Mwinula.
Mama Kikwete amemaliza jana ziara ya kikazi ya siku tatu katika mkoa wa Kagera yenye lengo la kuchangia juhudi za kupunguza vifo vya kinamama vinavyotokana na uzazi kwa kutoa vifaa vya huduma ya afya ya uzazi, hususan katika wodi za wazazi. Kuhamasisha juhudi za maendeleo kwa wanawake kupitia vikundi vya SACCOS na benki za vijijini- VICOBA.
Kuhamasisha juhudi za kupunguza matukio ya mimba na utoro mashuleni, kuhamasisha vikundi vya SACCOS na benki za vijijini- VICOBA na kuhamasisha juhudi za kupunguza matukio ya mimba na utoro mashuleni.

You liked this post? Subscribe via RSS feed and get daily updates.

0 comments:

Post a Comment