Waumini wa kkkt usharika wa mtongani watoa msaada katika hospitali ya temeke

Hidaya Utawangu ambaye ni Afisa Muuguzi wa hospitali ya wilaya ya Temeke akivihesabu vyandarua 100 walivyopewa na waumini wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) usharika wa Mtoni Mtongani baada ya kuwapatia vyandarua 100 kwa ajili ya kutumika katika wodi za hospitali hiyo .

Na Anna Nkinda
29/12/2008 Dar es Salaam Waumini wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Usharika wa Mtoni Mtongani wamewaomba wananchi wenye uwezo kuwakumbuka wagonjwa na watu wasiojiweza kwa kuwapa misaada mbalimbali ambayo itawafariji na kuwasaidia katika maisha yao.
Waumini hao waliyasema hayo hivi karibuni walipowatembelea na kutoa misaada mbalimbali kwa wagonjwa waliolazwa katika hospitali ya Wilaya ya Temeke ikiwa ni sehemu mojawapo ya kusherehekea sikukuu ya Christimas.
“Kanisa letu linatoa huduma mbalimbali za kijamii hivyo basi huduma hii tunayoitoa leo ni mojawapo ya huduma tunazozitoa ila huwa tunawahudumia wagonjwa waliopo majumbani lakini leo kwa mara ya kwanza tumeweza kuwahudumia na wagonjwa waliolazwa Hospitalini”, walisema waumini hao kwa furaha.
Mchungaji wa Kanisa hilo Leah Mwankenja ambaye alikuwa ni Kiongozi wa msafara huo alisema kuwa ni agizo la Bwana Yesu wanahuduma na kuwafariji wagonjwa hivyo basi nao wameona kwa kipindi hiki cha sikukuu watimize agizo hilo.

Mchungaji huyo aliendelea kusema kuwa huduma hiyo itakuwa endelevu na kuwataka watu wenye uwezo na afya njema watumie baraka za Mungu kuwajali wahitaji.

Naye Hidaya Utawangu Afisa Muuguzi wa hospitali hiyo ambaye pia siku ya tukio alikuwa ni msimamizi wa zamu aliwashukuru waumini hao kwa msaada walioutoa kwani katika mkoa wa Dar es Salaam hospitali ni nyingi hivyo basi kwa kuwafikiria wao ni upendo wa kipekee.

Afisa huyo alisema kuwa vyandarua walivyopewa vitasaidia sana ingawa ni vichache kutokana na mahitaji ya hospitali kwani vitanda ni zaidi ya vyandarua walivyopewa hivyo aliziomba Taasisi za kiserikali na zisizo za kiserikali , watu binafsi na mashirika ya umma wawapatie msaada pindi watakapopata nafasi.

Alimalizia kwa kusema kuwa taratibu za kwenda kuwatembelea wagonjwa na kutoa msaada hospitalini hapo ni kuandika barua ya maombi utawala ukishakubaliwa unapangiwa siku nzuri yenye nafasi.

Aidha wagonjwa waliolazwa hospitalini hapo waliwashukuru waumini hao kwa kitendo cha kuacha kufanya starehe kama wafanyavyo wengine na kwenda kusherehekea sikukuu pamoja nao .
“Tumepata faraja kubwa sana kwani kwa kawaida anapokuja kukuona mtu ambaye hamfahamu na kukupa pole unafarijika kwa kuwa ni kitu ambacho hukukitegemea”, walisema wagonjwa hao.
Waumini hao walitoa vyandarua 100 ambavyo vitatumika mawodini, sabuni za kufulia na kuogea, biskuti, pipi, juice ambazo waliwakabidhi wagonjwa waliokuwa wamelazwa katika wodi za wazazi, wanawake, watoto na wanaume.

You liked this post? Subscribe via RSS feed and get daily updates.

0 comments:

Post a Comment