CHAMA CHA MPIRA WA NETIBOLI NCHINI CHAOMBA UDHAMINI NA MISAADA KWA WADAU WA MICHEZO!!

Mwenyekiti wa chama cha Netiboli nchini Anna Bayi kushoto akiongea mbele ya waandishi wa habari kwenye ukumbi wa idara ya habari maelezo leo, kuzungumzia mikakati ya chama hicho katika kuendeleza mchezo huo nchini, katikati ni Shyrose Bhanji makamu mwenyekiti na mwisho ni Rose Mkisi katibu msaidizi.

MAELEZO YA MWENYEKITI WA CHAMA CHA MPIRA WA NETIBOLI NCHINI – CHANETA- ANNA BAYI KATIKA KIKAO CHA UONGOZI MPYA WA CHANETA NA WAANDISHI WA HABARI – UKUMBI WA MAELEZO- DSM 23/12/2008.
Awali ya yote nichukue fursa hii kuwashukuru kwa dhati kwa kuitikia wito wetu wa kukuta leo hii na uongozi mpya wa CHANETA ambao uliingia madarakani tarehe 6/12/2008. ASANTENI SANA.
Tumeona ni vema kupitia kwenu tuweze kujitambulisha rasmi sisi viongozi tuliochaguliwa na vile vile kuelezea mikakati ya muda mrefu na muda mfupi na mipango ambayo tunadhani itasaidia mchezo huu wa netiboli kupiga hatua. ( UTAMBULISHO)
Kwanza kabisa lazima tukiri kwamba CHANETA ina mikakati mingi na mizuri, lakini kikubwa ambacho tunahitaji ni misaada pamoja na udhamini toka kwa wadau mbalimbali ili kuangalia jinsi ganI tutasaidiana kuziba pengo la ukata ndani ya CHANETA.
Tunawaomba wadau wa mchezo huu, wale wasio wadau, wapenzi wa mchezo huu na watanzania kwa ujumla kujitokeza kwa hali na mali kusaidia chochote walichonacho kwa ajili ya kuuendeleza mchezo huu. Tutashukuru sana iwapo kila mtanzania kwa nafasi yake atauunga MKONO juhudi zetu CHANETA, ili wote kwa pamoja tusaidiane kuuendeleza mchezo huu.
Vile vile ni Imani yetu kwamba wadhamini mbalimbali, iwe ni makampuni binafasi au mashirika mbalimbali yataitikia wito wetu ili wajitokeze kwa ajili ya kudhamini mashindano mbalimbali ambayo yapo kwenye kalenda yetu ya mwaka kesho. Sisi pia tunawaahidi kwamba kampuni yoyote itayojitokeza kudhamini michezo yetu, timu zetu zitapata ari na moyo kama vile ilivyokuwa katika timu ya taifa ya soka- Taifa Stars.
Tunaomba viongozi wa ngazi zote kuanzia ngazi ya Serikali ya Mitaa, Wilaya, Mikoa na Taifa nao waunge mkono juhudi zetu na watusaidie kwa hali na mali na vile vile kuamsha ari ya mchezo huu ili uweze kupendwa na wadau mbalimbali.
Moja ya changamoto kubwa iliyoko mbele yetu ni kutafuta pesa kwa ajili ya mashindano mbalimbali yakiwemo ya Taifa yanayotarajiwa kufanyika mwezi Aprili mwaka kesho huko mkoa wa Pwani. Mengine ni ligi daraja la kwanza ambayo yatashirikisha club 18, na ligi daraja la pili Taifa inayoshirikisha klabu bingwa za nchi zote. Vile vile kutakuwa na ligi za wilaya na mikoa.
Mwezi February, 2009 pia tunatarajia kuzindua rasmi kambi ya maandalizi ya mashindano ya timu ya Vijana U-21 yanayotarajiwa kufanyika Windhoek, Namibia mwezi March na Aprili 2009. Mashindano haya yanafanyika mara ya kwanza ili kuwaandaa vijana kwa ajili ya mashindano makubwa zaidi ya kimataifa. Mashindano haya yatashirikisha nchi zote za AFRICA ambao ni wanachama wa CANA) Conferederation of African Netball Associations. Tanzania ni mwanachama hai wa CANA.
Gharama zinazohitajika ni usafiri wa kuipeleka timu ya netiboli nchini Namibia kwenye mashindano haya, pamoja na gharama za vifaa na gharama zingine kwa ajili ya maandalizi ya kambi.
Kwa kumalizia ni Imani yetu vyombo vya habari vitatusaidia kuwahabarisha watanzania kuhusu maombi yetu ya kuomba misaada ya hali na mali na udhamini wa mashindano mbalimbali kwa lengo ya kuendeleza mchezo huu.

You liked this post? Subscribe via RSS feed and get daily updates.

0 comments:

Post a Comment