WAKENYA WAFANYA MASHINDANO YA MPIRA WA MIGUU KUHAMASISHA AMANI!!


Na Anna Nkinda - AMWIK
Maiella Kenya.

Mpira wa miguu ni mchezo ambao unapendwa na watu wengi Duniani wakiwemo wakubwa, vijana, watoto, wanawake kwa wanaume. Ni mchezo ambao unawaunganisha na kuwaleta watu pamoja.

Kutokana na tatizo la ukosefu wa amani lililokuwepo kwa muda mrefu katika tarafa ya Maiella wilayani Naivasha mkoa wa Bonde la Ufa ni mwaka wa pili sasa mashindano ya amani yanafanyika ili kuwaunganisha na kuwaleta pamoja wakazi wa eneo hilo.

Hivi karibuni mashindano ya mpira wa miguu ya amani yalifunguliwa kwa mara ya pili na mhasibu wa chama cha waandishi wa Habari wanawake Nchini Kenya (AMWIK) Moses Masawa.

Mchezo huo ni baadhi ya mbinu ambazo AMWIK inatumia katika mradi wake wa kuimarisha amani katika mkoa wa Bonde la Ufa ambao ulikumbwa na vita na ghasia kutokana na kura ya jumla ya mwaka 2007. Mradi huo unafadhiliwa na wakfu wa Ford (Ford Foundation)

Kabla ya kufungua mashindano hayo yaliyoanza tarehe 17/7/2010 Masawa aliwakabidhi viongozi wa timu kumi ambazo zinaashiriki mashindano hayo mipira yenye thamani ya Kshs. 14,500 pamoja na vifaa vya huduma ya kwanza viwili vyenye thamani ya Kshs. 2400/=.

Masawa aliwataka wachezaji hao kucheza kwa amani na upendo ili kuimarisha amani ambayo hivi sasa imeanza kurejea katika eneo hilo.

Aliwahimiza wananchi hao kuishi kwa umoja kwani wote ni wakenya tofauti ya makabila waliyokuwa nayo isiwafanye waishi kwa kuchukiana.

Naye Mwenyekiti wa Mashindano hayo James Ole Omelai alisema kuwa hii ni mara ya pili kuandaa mashindano kama hayo ambapo kwa mara ya kwanza yalifanyika mwaka jana.

Alisema kuwa mashindano hayo yamesaidia kwa kiasi kikubwa kuwaleta wakazi wa kata hiyo pamoja na hivyo kudumisha amani na maelewano baina yao.

Alizitaja timu ambazo zinazoshiriki katika mashindano hayo kuwa ni home boyz, Valley Shooter, Green Eagle, Eleven Junior, Desert Warrior, Zion Football Club (F.C), Black Tigers F.C, Dynamo F.C , Nkampani F.C na Hammers F.C.

Mechi ya ufunguzi katika mashindano hayo ilianza baina ya timu za Homeboys na Valley Shooter ambapo timu ya Home boys iliibuka na ushindi wa mabao 3-2 .

Mshindi wa kwanza katika mashindano hayo ambayo yanafanyika katika uwanja wa mpira uliopo shule ya Msingi Maiella atapewa zawadi ya fedha taslimu Kshs. 8000/=, mshindi wa pili Kshs. 6000/=, mshindi wa tatu Kshs. 4000 na mshindi wa nne Kshs. 2000/=.
Mwisho.

You liked this post? Subscribe via RSS feed and get daily updates.

0 comments:

Post a Comment