WACHAFUZI NA WAHARIBIFU WA MAZINGIRA KATIKA BAHARI, MITO NA MABWAWA KUDHIBITIWA.



Na. Aron Msigwa – MAELEZO.


Serikali imewataka wananchi wanaoishi kuzunguka maeneo ya Bahari, Maziwa, mito na Mabwawa kutojihusisha na vitendo vya uharibifu na uchafuzi wa mazingira.Kauli hiyo ilitolewa jana wilayani Mafia na Katibu mkuu Wizara ya Maji na Umwagiliaji Christopher Sayi kufuatia kuzinduliwa kwa Mkakati wa Hatua za Haraka za Kuhifadhi Mazingira ya Bahari ukanda wa Pwani, Maziwa, Mito na Mabwawa.

Akizungumza na wananchi wa wilaya hiyo kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) Dkt. Batilda Burian alisema kuwa hali inayojitokeza sasa ya kupungua kwa ubora wa maji na hewa ya oksijeni pamoja na kutoweka kwa baadhi ya aina za samaki katika Bahari, maziwa, mito na mabwawa kunasababishwa na kuendelea kwa vitendo vya uchafuzi na uharibifu mkubwa wa mazingira vinavyofanywa na baadhi ya wananchi.

Alisema serikali tayari imeandaa mkakati wa kuhifadhi Mazingira ya Bahari, Ukanda wa Pwani, Maziwa, mito na Mabwawa unaoelekeza kuchukuliwa kwa hatua za haraka kukabiliana na vitendo vya uchafuzi na uharibifu wa mazingira katika maeneo yote husika nchini.

Akizitaja hatua mbalimbali zilizomo katika mkakati huo Bw. Sayi alisema kuwa ni pamoja na Ukomeshaji wa uvuvi haramu wa kutumia Baruti na Sumu,Uvuvi wa kutumia Nyavu zisizoruhusiwa, Uvuvi wa viumbe waliopo hatarini kutoweka na ukataji wa Misitu ya mikoko kandokando mwa bahari.

Hatua nyingine ni pamoja na uzuiaji wa ujenzi usiozingatia taratibu katika ukanda wa Pwani kandokando ya maziwa na umwagaji wa maji taka, utupaji wa taka ngumu, kuzuia uvamizi katika ardhi – Oevu, uzuiaji wa shughuli mbalimbali za kibinadamu zinazochangia kuchafua mazingira katika miinuko ya maziwa mito na mabwawa nchini pamoja na vitendo vya uchafuzi wa mazingira vinavyofanywa na jamii inayozunguka maeneo ya maziwa mito na mabwawa.

You liked this post? Subscribe via RSS feed and get daily updates.

0 comments:

Post a Comment