Na Joseph Ishengoma MAELEZO, DODOMA
Jumuiya ya Diaspora nchini Uingereza leo imetoa tuzo kwa Mhe Al Sheymaar Kwagyr kwa kutambua mchango wake wa kupambana na mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (maalbino).
Akikabidhi tuzo hiyo katika viwanja vya bunge mjini Dodoma, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watanzania nchini Uingereza Bwana Said Sururu amesema wametoa tuzo hiyo baada ya kuangalia jitiada aalizochukua tangu alipochaguliwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa mbunge. 

Amezitaja baadhi ya juhudi hizo kuwa ni kuanzisha mfuko wa Hope foundation uliomuwezesha kutembea nchi nzima akilaani mauaji ya albino. “Lakini pia yeye ni mlemavu wa ngozi, ameonyesha uwezo mkubwa na kipaji bila woga katika kupigania haki za watu wenye ulemavu wa ngozi,” amesema.
Bwana Sururu amesema, “Kutokana na juhudi zake, ameshirikiana na Watangazaji wa Shirika la Utangazaji la Uingereza na kuandaa makala iliyoonyeshwa na televisheni ya BBC, Uingereza ikielezea ukatili wanaofanyiwa watu wenye ulemavu wa ngozi.” Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo, huo ulikuwa mchango mkubwa katika kupambana na mauaji ya albino kwani Jumuiya ya Kimataifa iliweza kupata picha halisi ya ukatili wanaofanyiwa.
Hii ni mara ya pili kwa Diaspora, Uingereza kutoa tuzo kwa raia wa Tanzania. Mara ya kwanza ilikuwa Juni 18,2010 walipotoa tuzo kwa WAziri wa Afrika Mashariki Dr. Diodorus Kamala baada ya kutetea wananchi wa Tanzania katika masuala ya ardhi kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, Mhe. Al Sheymmar ameishukuru Diaspora kwa kutambua mchango wake na Kumshukuru RAis Kikwete kumchagua kuwa mbunge. “Naishukuru sana Jumuiya ya Diaspora kunipatia tuzo hii, namshukuru pia Rais Kikwete kwa kunichagua kuwa mbunge.
Nawaomba watanzania wote tuwe kitu kimoja kuhakikisha mauaji ya albino yanakomeshwa,” amesema. Hafla ya kukabishiwa tuzo hiyo imeudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo WAziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa Mhe Benard Membe.






0 comments:
Post a Comment