NA JOSEPH ISHENGOMAMAELEZO, Dodoma.
Mbunge wa jimbo la Kwera mkoani Rukwa Mh. Chrisant Mzindakaya ameliaga bunge baada ya kulitumikia kwa muda wa miaka 40 na kuvishutumu vyama vyote vya siasa nchini kwa kushiriki katika vitendo vya rushwa wakati wa uchaguzi.
Mhe. Dr. Mzindakaya aliyepewa upendeleo maalum jana na Spika wa Bunge Mhe Samwel Sitta kuchangia dakika 15 tofauti na wabunge wengine alisema kuwa hawezi kushiriki katika kuchangia miradi ya maendeleo ya jimbo lake arafu akatoa rushwa kwa wapigakura wake.
"Mimi siwezi kuchangia ujenzi wa madarasa alafu nikatoa Tsh 2,000 kulimpa mjumbe ili anipe kura. tabia hii ni mbaya sana na vyama vyote vimeshiriki katika uchafu huu," alisema huku wabunge wote wakimsikiliza kwa makini.
Dr. Mzindakaya aliyeingia bungeni tangu mwaka 1965 akiwa na umri wa miaka 25 alisema kuwa haondoki bungeni kwa uzee, "nataka kuondoka kwa upendo na amani, sitaki kuwa mbunge kwa kutumia pesa."
Alito wosia kwa bunge lijalo na kutaka liwe la uchumi badala ya kuendelea kuelekeza nguvu zaidi katika siasa kwasababu sifa ya siasa nchi inayo tangu enzi za Mwalimu Nyerere.
"Ni aibu sisi kusaidiwa na nchi kama Uholanzi iliyobadilisha bahari kuwa eneo la kilimo.
Tumieni sheria ya ubia kati ya serikali na makampuni binafsi kupunguza mwanya kati ya matajiri na maskini. Utajiri wa nchi hii unashikiliwa na watu wasiozidi 10. hapa tunatakiwa kupanga na pia hangaikeni kujenga kada ya watu wa chini, hawa wakubwa msihangaike nao watahangaika wenyewe," alisema.
Wakati wa utumishi wake, Dr. Mzindakaya aliyekuwa maarufu bungeni kwa kulipua mabomu wakati wa serikali ya awamu ya tatu, ameshikilia nyadhifa mbalimbali ikiwemo Ubunge, Naibu waziri wa Biashara na Viawanda, Mkuu wa mkoa wa Morogoro, Mbeya, Kigoma na Rukwa.
Kwa upande wake Mhe. Sitta alimshukuru sana kwa nasaha zake na kusema kuwa Dr. Mzindakaya wakati wa utumishi wake ni mtu aliyekuwa muwazi,, asiyeficha hisia zake na hakuwa mnafiki.
"Wanasiasa wa aina ya Dr. Mzindakaya sio wengi nchini. ni wakati wa kuangalia upya kanuni zetu ili watu kama hawa watoe hoja ili na vizazi vijavyo viweze kuzisoma katika hansad za bunge baadae ," alisema.
Wabunge wengine waliotangaza nia yao ya kutogombea tena ni pamoja na Paul Kimiti (Sumbawanga mjini) aliyelitumikia bunge tangu mwaka 1975.






0 comments:
Post a Comment