AJIRA MILIONI 1.3 ZAPATIKANA: MAKONGORO MAHANGA!!


MAGRETH KINABO NA BENJAMIN SAWE MAELEZODODOMA.

SERIKALI imesema kwamba jumla ajira 1,313, 561 zimepatikana katika kipindi cha mwaka 2006 hadi kufikia Desemba mwaka 2008 kwa sekta binafsi na Aprili mwaka huu kwenye sekta ya umma, ambapo sekta ya isiyorasmi inaongoza kwa asilimia 81.7 ya ajira zote.

Aidha katika sekta hiyo iliyoongoza wananchi wamejihusisha zaidi kwenye shughuli kama vile biashara ndogondogo na utoaji huduma. Hayo yalisemwa jana Bungeni na Naibu Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana Dk. Makongoro Mahanga wakati akijibu swali na Mbunge wa Bumbuli(CCM) William Shellukindo lililouliza kuwa ni maeneo gani ambayo yameongezeka ajira kwa asilimia katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi(CCM).

Akijibu swali hilo , Dk. Mahanga alisema ongezeko la ajira kwenye sekta isiyorasmi kunachangiwa na sababu ya urahisi wa kuanzisha shughuli ndogondogo ambazo zinahitaji mtaji mdogo, urahisi wa upatikanaji wa maligahafi, miradi kumilikiwa na kaya, mahitaji ya teknolojia taaluma na ushindani .

Alisema sekta binafsi inaongoza kwa kutoa ajira 1,185,387 sawa na asilimia 90.2 na Serikali imetoa ajira mpya 128,174 sawa na asilimia (9.8). Dk .Mahanga alizitaja sekta nyingine zilizozalisha ajira mpya ni ujenzi kwa asilimia 9.31 y a ajira zote, ikifuatiwa na elimu asilimia 2.97, afya asilimia 2.89, usafirishaji na mawasiliano asilimia 1.22, huduma za asilimi 0.61. Aliongeza kwamba mchanganuo wa ajira mpya kuhusu kilimo, uvuvi na ufugaji kiasilimia zinatarajiwa kutolewa mara baada ya zoezi la uchambuzi wa sensa ya kilimo iliyofanyika mwaka 2009 kukamilika. Naibu Waziri huyo alisema Serikali inategemea kufanya utafiti kuhusu kuhusu ajira gani zenye mvuto zaidi kwa Watanzania.

You liked this post? Subscribe via RSS feed and get daily updates.

0 comments:

Post a Comment