TAMKO LA CHAMA CHA NCCR-MAGEUZI KUHUSU MSONGAMANO WA MAGARI JIJINI DAR ES SALAAM!!

Mwenyekiti wa chama chama cha NCCR Mageuzi James Mbatia akizungumza na waandishi wa habari katika makao makuu ya chama hicho Ilala leo katikati ni katibu mkuu wa chama hicho Samuel Ruhuza na mwisho ni Mwenyekiti wa idara ya wanawake NCCR Mageuzi Amina Suleiman.
Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi James Mbatia akizungumza na mwanablogu John Bukuku nje ya ofisi hiyo mara baada ya kumalizika mkutano, kulia na Mwandishi kutoka gazeti la Changamoto Suleiman Msuya.

Leo Chama cha NCCR-MAGEUZI tumewaomba tukutane , ili tuweze kujadiliana kwa pamoja tatizo la msongamano wa magari katika jiji la Dar es Salaam.

Wengi tumekuwa tukizungumzia hali hii ya msongamano wa magari katika ngazi ya kero. Mvua ya masika inayonyesha sasa inatuonesha kwa vitendo, kwamba hali hii tuliyojitengenezea siyo kero tena bali ni tatizo linanohitaji utatuzi wa haraka katika muda mfupi na utatuzi wa muda mrefu.
Kwa kushirikiana na wanataaluma na wanaharakati wa mambo ya Mipango Miji, Afya ya Binadamu, Haki za Binadamu na Tabia nchi tumebaini kwamba hili ni tatizo la kitaifa. Hoja hii inajidhihirisha pia katika katika majiji mengine nchini. Kwa mfano jiji la Arusha na jiji la Mwanza nayo yameshaanza kukerwa na hali hii ya msongomano wa magari barabarani.

NCCR-Mageuzi tumetafakari na kuona kwamba tunahitaji kuweka nguvu zetu zaidi katika kupata utatuzi, kuliko kutumia muda katika kulalamika au kutafuta chanzo cha tatizo kwani inafahamika haya ni matokeo ya mifumo ya isiyojali utu, inayodumaza ustawi wan chi zinazojulikana kama nchi zinazoendelea.

Tunafahamu kwamba historia ya ujenzi wa majiji katika ukanda wa bahari katika nchi ambazo zinaendelea haitofautiani sana. Mfano ni majiji kama Lagos nchini Nigeria na Cape Town nchini Afrika Kusini, yalikumbwa au yanakumbwa na tatizo hili na wameweza au wanatafuta utatuzi wake.

Utatuzi endelevu kwa tatizo hili la jiji la Dar es Salaam itatokana na dhamira yetu ya pamoja kama taifa, inayojali masilahi ya wote bila ya kumsahau mama yetu dunia.

Masilahi ya wote ni muhimu. Kwani kwa kukokotoa takwimu endelevu tumeweza kubaini kwamba, kwa wastani kero hii ya msongamano wa magari katika jiji la Dar es Salaam inaligharimu taifa letu zaidi ya shilingi za Kitanzania bilioni 4 kila siku. Kiasi hiki cha thamani kinatokana na:

· Asilimia 30 ya muda wa Wanajiji la Dar es Salaam unatumika katika kusafiri kutoka na kurudi kwenye makazi yao kwa ajili ya kwenda kwenye shughuli binafsi au kazini;
· Nguvu ya ziada ya nishati inayotumika; na
· Hewa mkaa (carbon dioxide) ya ziada itokayo kwenye magari.

Gharama hii ya shilingi za Kitanzania bilioni 4 haijumuishi gharama ya msongo (stress) inayowakumba Wanajiji la Dar es Salaam, itokanayo na tatizo hili.

Mfano: Tukitumia ulinganisho, tunaona kwamba shilingi za Kitanzania bilioni 4 kwa siku, zinaweza kutumika kununua madawati 80,000 kwa bei ya shilingi 50,000 kwa dawati kwa matumizi ya watoto wetu. Au gharama ya kujenga Kituo kimoja cha Afya cha kisasa ni shilingi za Kitanzania bilioni 2. Hivyo kwa kutumia ulingano, kila siku tatizo hili la msongamano wa magari hapa jijini Dar es Salaam linatugharimu ujenzi wa vituo vya afya viwili vya kisasa. Ambapo huu ni ustawi hasi kwa taifa letu.

Takwimu hizi zinatuumbua tunapolalamika kila siku, kwamba sisi ni maskini. Takwimu hizi zinatupa nafasi ya kushirikiana katika kutafuta utatuzi wa tatizo hili. Tunaomba tuweke mbele masilahi ya pamoja kama tiafa katika kupata haraka utatuzi wa tatizo hili.

Leo NCCR-Mageuzi tunatoa mchango wetu kwa kutoa mapendekezo yafuatayo:-

1. Kusimamisha au kutoendelea kutoa vibali vya kujenga ofisi, maduka makubwa na madogo katikati ya jiji;

2. Wataalamu wetu wakutane mara moja ili kuboresha utaratibu uliopo wa usafiri jijini na wapewe nyezo za kukarabati miundo mbinu ya barabara zilizopo sasa;

3. Uwezekano upo wa kutumia treni kutoka Pugu – Gongolamboto – Vingunguti – Buguruni mpaka Kituo Kikuu cha Kati. Pia kutoka Ubungo mpaka Kituo Kikuu cha Kati;

1. Uwezekano upo wa kutumia njia ya Boti kutoka Bagamoyo – Mbweni – Tegeta – Mbezi – Msasani mpaka Bandarini;

2. Serikali igharamie mradi usio wa kibiashara wa mabasi ya kisasa kwa jiji la Dar es Salaam;

3. Ghala la kuhifadhi mizigo kutoka bandarini lijengwe nje ya jiji, kwa mfano Chalinze;

4. Soko Kuu la chakula lijengwe nje ya jiji, kwa mfano Kibaha;

5. Tunapendekeza ofisi zifuatazo zihamishiwe nje ya jiji au hata nje ya mkoa. Mfano Wizara ya Ardhi, Wizara ya Elimu, Wizara ya Mambo ya Ndani, Wizara ya Ulinzi, Wizara ya Utalii, Mahakama Kuu ya Tanzania, Magereza, na Makao Makuu ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania na uwanja wa ndege;

6. Kujenga eneo la kuengesha magari la kisasa lenye uwezo wa kuegesha zaidi ya magari 10,000; kwa mfano eneo la Jangwani; na

7. Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ifanyiwe kazi ili mfumo wetu wa sheria uweze kufanya kazi ipasavyo;

Ufafanuzi wa kina wa utekelezaji wa mapendekezo yetu upo, na tupo tayari kushirikiana na idara zinazohusika kwa utekelezaji. Kukata tamaa ni dhambi. Tunaomba tujitambue, kwamba Haki hupiganiwa. Uwezo wa kupata haki zetu tunao.
Aksanteni sana kwa kunisikiliza.
Mungu Ibariki Afrika !
Mungi Ibariki Tanzania !
Ndimi Mtumishi Mtiifu,

James Francis Mbatia
MWENYEKITI TAIFA

You liked this post? Subscribe via RSS feed and get daily updates.

0 comments:

Post a Comment