MAJESHI YA POLISI, MAGEREZA, UHAMIAJI NA ZIMAMOTO KUNUFAIKA NA HUDUMA YA MFUKO WA BIMA YA AFYA!!


Na Mohammed Mhina, wa Jeshi la Polisi

Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya nchini (NHIF) umeanza kutoa mafunzo kwa wakufunzi wa Majeshi ya Polisi, Magereza, Uhamiaji na Zimamoto ikiwa ni maandalizi ya kuwajumuisha askari hao katika huduma za matibabu hayo zinazosimamiwa na mfuko huo.
Mkurugenzi wa Usimamizi wa Mafao ya Mfuko wa Bima ya Afya nchini (NHIF) Dk. Frank Lekey, wakati akizungumza na Maafisa Wakuu wa Jeshi la Polisi na Askari wa vyeo mbalimbali kutoka Makao Makuu ya Jeshi hilo na Kanda Maalum ya Dar es Salaam.
Dk. Lekey amesema kuwa kuanzia Mwezi Julai mwaka huu, Mfuko huo utaanza kutoa huduma za matibabu kwa askari wa majeshi hayo kupitia katika Hospitali mbalimbali za Majeshi ya Polisi na Magereza.
Amesema kuanza kwa huduma hiyo kwenye Majeshi hayo, kunatokana na Bunge kuridhia mapendekezo ya mswada wa kuwajumuisha Askari Polisi, Magereza, Uhamiaji na Zimamoto na Uokoaji katika mpango wa kupatiwa matibabu kupitia mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya.
Akiwaelimika Makamanda na askari hao kuhusiana na huduma za Mfuko huo, Dk. Lekey amesema kuwa huduma hiyo itakapoanza kutolewa kwa askari hao ambao sasa wanakuwa ni sehemu ya wanachama wake, itakuwa ikitoa matibabu bila ya ukomo wa gharama.
Amesema Mfuko huo utaendelea kutoa matibabu hayo ili mradi tiba hiyo iwe inafuata miongozo ya makubaliano yaliyopo kwenye mkataba kati ya mfuko huo na mwanachama bila kujali ukubwa wa tatizo la mgonjwa.
Huku akishangiliwa na maafisa na askari hao Dk Lekey alisema, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya NHIF haujaweka ukomo wa matibabu kwa mwanachama kwa vile msingi unaondesha mfuko huo unataka kumtibia mwanachama hadi atakapo pona kabisa ama kufariki.
Hata hivyo amesema kuwa mfuko huo hautaweza kulipia gharama za matibabu kwa Mwanachama wake atakayeamua kujipatia tiba ya dawa za kuongeza ama kupunguza ukubwa wa maumbile ya mwili wake ama pale zitakapomletea madhara.
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Inspekta Jenerali Saidi Mwema, amewaagiza Makamanda wa Polisi wa Mikoa na Vikosi vyote Tanzania Bara na Visiwani, kuwahamasisha askari wote waliochini yao ili kujiunga na mfuko huo.
IGP Mwema amesema kuwa mfuko huo utakuwa ni ukombozi sio kwa askari wenyewe tu bali pia hata kwa wategemezi wao wakiwemo wake ama waume zao na watoto

You liked this post? Subscribe via RSS feed and get daily updates.

0 comments:

Post a Comment