WANAWAKE WA TABORA WAKUTANA KUJADILI UTEKELEZAJI WA AZIMIO LA ULINGO WA BEIJING!!

Katika picha ni washiriki wa Kongamano la Wanawake Wakiashiria kuridhia Maazimio ya Mkutano wa Beijing uliofanyika Miaka 15 iliyopita.

Na Asteria Muhozya, Tabora
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto Mhe. Margaret Sitta amevitaka vyama vya siasa nchini kuwasaidi wanawake wenye utoshi wa kisiasa kufikia azma zao.
Ameyasema hayo leo Mkoani Tabora katika ukumbi wa Chuo cha Veta wakati akifungua kongamano la Siku ya Wanawake Duniani kuelekea kilele cha Maadhimisho ya siku ya wanawake duniani tarehe 8 Machi,2010.
Mhe. Margaret Sitta ameongeza kuwa, ushiriki wa wanawake katika ngazi ya siasa unatokana na utashi wa kisiasa na hivyo lazima vyama vya siasa visaidie kufikisha azma hiyo.
Akielezea madhumuni ya kongamano hilo ameeleza kuwa, kongamano hili lina lengo la kujadili utekelezaji wa maeneo ya Azimio la Ulingo wa Beijing baada ya Miaka 15 ili kuanisha mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa Ulingo huo wa Beijing, kuanisha changamoto na kubainisha mikakati ya kukabiliana na changamoto hizo hususani katika maeneo manne ya kipaumbele yaliyobainishwa na Taifa ambayo ni kuwajengea wanawake uwezo wa kisheria,kuongeza ushiriki wa wanawake katika ngazi za maamuzi,kuwawezesha wanawake kielimu,mafunzo na ajira na kuwawezesha wanawake kiuchumi na kuondoa umaskini.
Aidha, Mhe, Margaret ameongeza kuwa, suala la wanawake limekuwa likijitokeza sana yanapozungumziwa masuala ya jinsia kwasasabu wanawake ni kundi kubwa ambalo bado liko nyuma sana katika maendeleo na ikizingatiwa kuwa wanawake ni asilimia 51 ya watu hapa nchini na kuongez kuwa, bila kuwazungumzia wanawake ina maana kwamba maendeleo endelevu na ya kweli hayazungumziwi na kufikiwa.
Akieleza vikwazo ambavyo vimekuwa vikimkwamisha mwananmke ameeeleza kuwa, vitendo vya kikatili ambavyo vinaendelea kwa kasi nchini imekuwa sababu mojawapo ya vikwazo vya kimaendeleo kwa mwanamke. Aidha, ameongeza kuwa, vitendo hivi vimekuwa vikididimiza hali za wanawake.
Aidha, ameeleza kuwa, mila na desturi potofu zimekuwa pia kikwazo kwa maendeleo ya mwanamke kwani hazimpi nafasi mwanamke katika kupanga na kushiriki kikamilifu katika shughuli za kumletea maendeleo yake mwenyewe na kujiendeleza katika nyanja mbalimbali.
Aidha, amewataka wananchi wa Tabora wanaoshiriki katika kongamano hili kuongeza weledi wa masuala ya Jinsia na Wanawake ili kuleta maendeleo ya kweli kwa mwanamke na Taifa kwa ujumla.
Akizitaja mada zitakazo wasilishwa katika kongamano hilo la siku moja amesema kuwa, ni namna gani ya kuongeza ushiriki wa wanawake katika ngazi za maamuzi,kuwawezesha wanawake kiuchumi, kuwapatia wanawake elimu , mafunzo na ajira, kupiga vita ukatili dhidi ya wanawake, watoto na albino na akaeleza kuwa, Mkoa wa Tabora pia utatoa uzoefu wake katika utekelezaji wa shughuli za wanawake Mkoani humo.
Kwa upande wa washiriki wa kongamano hilo, wameeleza kuwa, mara baada ya kongamano hilo kumalizika wamependekeza yafuatayo yatekelezwe; Changamoto zinzowakabili wanawake zishughulikiwe, wanawake vijijini wawezeshwe kiuchumi na kielimu. Aidha, wamewataka wanaume kusaidia kuhamasisha mfumo wa utu na kukomesha mfumo dume.
Aidha, pamoja na hayo wametaka pia kutoka na mkakati wa pamoja wa kushugulikia changamoto zilizopatikana wakati wa utekelezaji wa Azimio la Ulingo wa Beijing.
Kongamamno hilo linawashirikisha wadau wanwake na wanaume kutoka katika wizara za Serikali, Taasisi za Serikali, vyama vya Siasa, Vyama vya Kiraia, Mashirika Yasiyo ya Kiserikali na wawakilishi wa vikundi mbalimbali vya wanawake na wawakilishi wa dini mbalimbali.


You liked this post? Subscribe via RSS feed and get daily updates.

0 comments:

Post a Comment