NA MAGRETH KINABO – MAELEZO
SERIKALI imesema, kilimo cha umwagiliaji ndio mkombozi wa uhakika na usalama wa chakula nchini , hivyo wananchi hawana budi kukipa kipaumbele ili kuweza kuboresha maisha na kujiongezea kipato.Hayo yalisemwa juzi jioni na Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Profesa Mark Mwandosya wakati wa sherehe za kuukaribisha mwaka mpya na kuwaaga wastaafu zilizofanyika katika viwanja vya wizara hiyo jijini Dar es Salaam.“Wananchi wanatakiwa kuongeza jitihada katika kilimo cha umwagiliaji ili kikue kutoka asilimia moja kufikia asilimia 20,” alisema Profesa Mwandosya. Waziri Mwandosya alisema Baraza la Mawaziri limeshapitisha Sera ya Taifa ya Umwagiliaji hivi karibuni, ikiwa ni hatua ya uboreshaji wa Kilimo cha Umwagiliaji.Profesa Mwandosya alimshauri Katibu Mkuu Mstaafu wa wizara hiyo,Wilison Mukama kuandika kitabu juu ya uzoefu wake katika utendaji kazi serikalini ili kiweze kuwa funzo kwa watumishi wengine.Pia alimshauri Mkurugenzi mstaafu wa Uchimbaji Visima na mabwawa Dk.Akbar Mohamed kuandika kitabu cha uchibaji visima Tanzania huku akimsifia kuwa amebobea kwenye utaalamu huo,ambapo kwa kuangalia mchanga anaweza kutambua sehemu husika hakuna maji.Naye Katibu Mkuu wa wizara hiyo Christopher Sayi, aliwapongeza wastaafu wa Wizara hiyo kwa kazi nzuri waliyofanya na kuwaasa watuimishi wengine kuiga mfano wao.Akimzungumzia utendaji wa Mukama, Sayi alisema amejifunza mambo manne, ambayo ni kutoa majalada kwa wakati, msikivu kwa watumishi wengine na kupata ushauri ili kuweza kutoa maamuzi mazuri.Mengine ni kujali maslahi ya wafanyakazi na kuwa makini katika kufuata sheria na na taratibu za kazi ili kuweza kupunguza matatizo sehemu za kazi. Wakati Mukama aliwatoa hofu watumishi wengine kuacha kuogopa kustaafu kwani ni jambo zuri kwa vile hutoa nafasi kwa wengine. Aliipongeza wizara hiyo kwa utendaji kazi mzuri wakati rasilimali walizonao ni chache.
0 comments:
Post a Comment