SERIKALI YAWABANA WAHAMIAJI HARAMU NCHINI!!


(Na Veronica Kazimoto – MAELEZO)
Dar es Salaam
16.02.2010.
Idara ya Uhamiaji imekamata wahamiaji haramu elfu tano ndani ya kipindi cha miaka miwili (2008 – 2010) wakitokea nchi za Burundi, Kenya, Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Somalia na Ethiopia. Kati yao wahamiaji wapatao elfu tatu wamefukuzwa nchini.
Kwa mujibu wa taarifa ya msemaji wa Idara hiyo Bwana Abdi Ijimbo, wahamiaji wengine elfu mbili baadhi yao kesi zao ziko mahakamani kwa ajili ya kuchukuliwa hatua za kisheria. Endapo watabainika kukiuka sheria za uhamihaji wanaweza kukabiliwa na kifungo, kurudishwa makwao au kutakiwa kuhalalisha ukaaji wao nchini.
Taarifa hiyo imefafanua kuwa, wahamiaji wengi waliokamatwa na Idara hiyo wametokea nchi za Pembe ya Afrika, yaani Ethiopia na Somalia wakitumia nchi ya Tanzania kama kipenyo cha kuelekea nchi za kusini mwa Afrika.
Taarifa hiyo imeendelea kubainisha kuwa, katika kipindi cha 2007 hadi 2008, kulikuwa na wimbi kubwa la wahamiaji haramu waliongia nchini Tanzania kupitia Kenya na Uganda wakielekea nchi za kusini mwa Afrika. Wengi wao wahamiaji hao walikuwa wanaume wenye umri kati ya miaka 20 hadi 45.
Taarifa hiyo imezitaja sababu zinazopelekea kuwepo kwa wimbi kubwa la wahamiaji haramu kuwa ni pamoja na machafuko ya kisiasa yanayozikabili nchi za Somalia na Ethiopia. Sababu nyingine zinahusu matatizo ya kiuchumi yanayozikabili nchi hizo pamoja na imani waliyonayo vijana kuwa maisha mazuri hupatikana Afrika Kusini na nchi za ulaya.
Idara ya uhamiaji imeanzisha Chuo cha Uhamiaji kijulikanancho kama Tanzania Regional Immigration Training Academy (TRITA). Chuo hiki kitatoa mafunzo kwa watendaji wa Idara za Uhamiaji katika nchi zinazoizunguka Tanzania.
Idara ya Uhamiaji inawaomba wananchi kutoa ushirikiano katika kufichua wahamiaji haramu pindi wanapobainika ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria mapema iwezekanavyo.

You liked this post? Subscribe via RSS feed and get daily updates.

0 comments:

Post a Comment