DK. MWINYI ATAKA BARAZA LIPAMBANE NA ADUI RUSHWA N A UKIMWI!!

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt. Hussein Mwinyi akionyesha kipeperushi wakati wa uzinduzi wa Mkataba wa Huduma kwa Mteja jijini leo kwa wajumbe wa Baraza kuu la wafanyakazi wa Wizara ya Ulinzi na jeshi la Kujenga Taifa.(kulia) Ni Mnadhimu Mkuu Jeshini Lt. Jenerali Abdulrahman Shimbo.Picha na Mwanakombo Jumaa -Maelezo.
NA MAGRETH KINABO – MAELEZO
BARAZA jipya la wafanyakazi wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, limetakiwa kuwa mstari wa mbele katika kupambana na tatizo la rushwa na Ukimwi ili kuweza kuimarisha maadili ya watumishi wa umma.
Agizo hilo lilitolewa jana na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk.Hussein Ali Mwinyi wakati wa uzinduzi wa baraza hilo , uliofanyika jijini Dar es Saalam, ambapo alisema rushwa na Ukimwi ni maadui hatari katika katika nchi yetu na sehemu kubwa ya ulimwengu.“Adui rushwa, huzaa upendeleo kazini, ufisadi wa mali ya umma, mapenzi holela katika sehemu za kazi na ubinafsi ambavyo huchangia kwa kiasi kikubwa kuporomoka kwa maadili ya utumishi wa umma.“Aidha adui Ukimwi yeye anaweza kuifuta wizara yetu kwa kuwaangamiza kidogokidogo watumishi wa umma, wapiganaji na maafisa wetu katika majeshi yetu. “Nawaombeni wote tubadili tabia ya kuwa na wapenzi wengi na tuimarishe ngono salama kwa ajili ya kulinda afya zetu na wenzetu,” alisisitiza Dk.
Mwinyi.Dk. Mwinyi aliwalitaka wajumbe wa baraza hilo, kuondoa dhana potofu ya kubaguana kwa kusema wafanyakazi fulani ni bora kuliko wafanyakazi wa aina nyingine na kuona kuwa wote ni kitu kimoja kama ulivyo mkono na vidole vyake vitano ambayo hutegemeana kwa kila jambo.Aliongeza kwamba majukumu ya baraza la wafanyakazi kulingana na Waraka wa Agizo la Rais Namba 1 la mwaka 1970 ni kushauri uongozi na kupanga sera bila ya malumbano. Wakati huohuo, Dk. Mwinyi alizindua Mkataba wa Huduma kwa Mteja ambao utawawezesha watumishi wa wizara hiyo kutoa huduma zenye ubora zaidi.
Dk. Mwinyi alisema umuhimu wa kuanzishwa kwa mkataba huo ni kuwawezesha wateja na wadau wao kufahamu aina na viwango vya huduma zitakazotolewa na wizara hiyo kwa wakati na jinsi ya kuzipata.Aidha kwa kupitia mkataba huo, wizara hiyo itapata mrejesho wa hudumazake ili kuweza kuziboresha.

You liked this post? Subscribe via RSS feed and get daily updates.

0 comments:

Post a Comment