Athari za mazingira zinazingatiwa kabla ya ujenzi wa Hotelli ya Kitalii!!

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Ezekiel Maige.
Na Tiganya Vincent, MAELEZO, Dodoma
Serikali imesema kwamba tathmini za kimazingira zimekuwa zikifanyika kabla ya kutolewa vibali vya ujenzi wa hoteli za kitalii ambapo hatua huchukuliwa kwa ujenzi unaofanywa kinyume cha utaratibu.
Pamoja na hatua Serikali pia imeendelea kuwaelimisha wawekezaji wapya na wa zamani wa sekta ya Hoteli za kitaalii umuhimu wa kuzingatia ubora ili kuhakikisha kuwa hoteli zinazojengwa zinakuwa na ubora unakubalika ndani na nje ya nchi.
Hatua hiyo inafuatia Wizara ya Maliasili kupata vigezo vinavyoonyesha na kugawa daraja za nyota kwa Hoteli za kitalii vilivyoandaliwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Kauli hiyo ilitolewa jana Bungeni mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Ezekeil Maige wakati akijibu swali la Mbunge Viti Maalum (CCM) Cynthia Ngoye aliyetaka kujua hatua zinazochukuliwa katika kudhibiti wageni na wasio wageni wanaojiita kuwa wawekezaji wa hoteli za nyota kuchukua ardhi ya wananchi kando kando ya Bahari Hindi na kujenga Hoteli za gharama ndogo na kuezeka kwa makuti.
Aliongeza kuwa Serikali itaendelea kutoa ushauri kwa wawekezaji katika hoteli za kitalii ili kuhakikisha kuwa huduma zinazotolewa zinalingana na daraja lake na sio vingingevyo.
Maige alisema kuwa Wizara hiyo ufanya ukaguzi wa hoteli zilizokamilika na kuziweka katika daraja na kisha taarifa huwasilishwa katika Kituo cha Uwekezaji(TIC) ili kuhakikisha kuwa uwekezaji umefanyika kwa mujibu wa mikata ya uwekezaji.
Aidha , Naibu Waziri huyo alisema kuwa suala la uezekaji wa kutumia makuti katika hoteli huzingatia zaidi aina ya hoteli inayojengwa , pamoja na madhari ya eneo na kuongeza kuwa uwekezaji wa makuti sio nafuu kama wengi wanavyodhani na unafaida nyingi za kimazingira.
Kwa upande mwingine Naibu Waziri huyo aliliambia Bunge kuwa ni jukumu la kila Mkoa hapa nchini kuainisha maeneo ya vivutio vya utalii kwa ajili kuvitafutia wawekezaji watakaosaidia kuweka miradi itakayowavutia watalii kutoka nje nandani ya nchi kutembelea maeneo husika.

You liked this post? Subscribe via RSS feed and get daily updates.

0 comments:

Post a Comment