Wanafunzi 592 wameacha shule wilayani Nkasi kwa kipindi cha miaka miwili!!

Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akisalimiana na wanafunzi katika moja ya shule alizowahi kuziutembelea.
Na Anna Nkinda - Maelezo, Nkasi
31/10/2009 Wanafunzi 592 wameacha shule wilayani Nkasi kutokana na tatizo la utoro, mimba, kukosa mahitaji na kuugua kwa kipidi cha miaka miwili na hivyo kusababisha kupungua kwa idadi ya wanafunzi wanaomaliza elimu ya shule ya msingi na sekondari wilayani humo.
Hayo yamesemwa jana na Mkuu wa wilaya hiyo Joyce Mgana wakati akisoma taarifa ya utekelezaji wa shughuli za maendeleoa ya wilaya kwa Mke wa Rais Mama Salma Kikwete aliyepo ziara ya kikazi ya siku tatu wilayani humo.
Mgana alisema kuwa tangu mwaka 2008 hadi sasa wanafunzi wa shule ya msingi alioacha masomo ni 226 kati ya hao wasichana ni 102 na wavulana 124 na katika shule za sekondari wanafunzi 366 waliacha masomo wakiwemo wasichana 195 na wavulana 171.
"Kuanzia mwaka 2008 hadi sasa wanafunzi 17 wa shule za msingi na wanafunzi 69 kwa upande wa sekondari walipata ujauzito na kesi zao zinaendelea mahakamani, kitendo hiki kinasababisha kwa kiasi kikubwa kushusha maendeleo ya mtoto wa kike", Mgana alisema.
Ili kukabiliana na tatizo la wanafunzi wa kike kupata ujauzito wilaya hiyo iko katika mkakati wa kujenga Hosteli mpya za wasichana zisizopungua tano kwa kila mwaka hadi sasa jumla ya Hosteli saba zinatarajiwa kukamilika kujengwa katika mwaka 2009/ 10.
Mkuu wa wilaya hiyo alisema kuwa, "Kuhusiana na tatizo la utoro mashuleni wanafunzi katika wilaya hii wanakula chakula cha mchana shuleni jambo ambalo limesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza tatizo hili".
Wilaya hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali katika sekta ya elimu ikiwa ni pamoja na ongezeko la watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu kwani hadi sasa katika shule za msingi kuna watoto yatima 4766 kati yao wasichana ni 2362 na wavulana 2404
Kwa upande wake Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) aliwataka wakazi wa wilaya hiyo kuhakikisha kuwa watoto wao wanasoma na kufuatilia maendeleo yao mashuleni.
"Ninawasihi kina baba na kina mama msipokee mahari ya watoto wenu msubiri hadi matokeo ya mtihani yametoka kama mtoto amefeli na mzazi anao uwezo wa kumsomesha katika shule ya kulipia ni bora ukampeleka mwanao shuleni kuliko kumuoza jambo ambalo litarudisha nyuma maendeleo yake ", alisema Mama Kikwete.
Aliendelea kusema kuwa Serikali ina makusudi ya kuanzisha shule za Sekondari za kata na kuongeza idadi ya shule za Msingi ili watoto wetu wasome na kupata wataalamu wengi ambao watasaidia kupunguza tatizo la wataalamu tulilonalo hivi sasa.
Wilaya hiyo ina shule za msingi 97 na shule za sekondari za Serikali 18 zilizojengwa kwa kushirikiana na wananchi, jumla ya wanafunzi katika shule za sekondari ni 6066 wasichana 2053 na wavulana 4013 na katika shule za msingi ni 49,428 kati ya hao wavulana ni 24,682 na wasichana ni 24,746.
Taasisi ya WAMA ilivichangia vikundi vya wanawake wajasiriamali vilivyopo wilayani humo Tshs. 1,500,000/= na Umoja wa Wanawake (UWT) Tshs. 500,000 fedha ambazo zitatumika kuinua mitaji ya vikundi hivyo.

You liked this post? Subscribe via RSS feed and get daily updates.

0 comments:

Post a Comment