MAMA SALMA KIKWETE AWATAKA WANAWAKE NCHINI KUCHAGUA VIONGOZI WANAOFAA!!

Mke wa Rais mama Salma Kikwete.

Na Anna Nkinda - Maelezo, Kilombero
23/10/2009 Wanawake nchini wametakiwa kushirikiana kwa pamoja ili waweze kuwachagua viongozi mahiri ambao atawaletea maendeleo katika uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji unaotarajia kufanyika mapema jumapili hii.
Wito huo umetolewa jana na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akiongea kwa nyakati tofauti na wanachama wa Umoja wa Wanawake wa Tanzania (UWT) katika wilaya za Mvomero, Ulanga, Kilombero na Kilosa.
Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema kuwa kila mtu anahaki ya kumchagua kiongozi anayemtaka hivyo basi kujitokeza kwa wingi kwa wanawake kupiga kura ndiko kutakakosaidia kumchagua kiongozi ambaye ataleta maendeleo na si kiongozi jina.
"Ninyi kama wanawake mnatakiwa kuangalia ni kiongozi wa Chama gani anayeweza kuitunza amani iliyopo hapa nchini kwani kuna baadhi ya watu wanapita na kuwadanganya kuwa njooni huku ni kuzuri ila mkumbuke kwamba amani ikipotea katika familia na katika nchi mtu wa kwanza kuathirika ni mwanamke", alisema.
Kwa upande wa kuongeza idadi ya wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mwenyekiti huyo wa WAMA aliwataka wanawake hao kuhakikisha kuwa idadi ya wanachama inaongezeka kwa wanawaleta wanawake wenzao ambao si wanachama wa UWT katika umoja huo.
Mama Kikwete alisema, "Kuanzia sasa rafiki wa mwanamke awe ni mwanamke mwenzake, mkumbushane katika kulipia kadi za uwanachama kwani kuna baadhi yenu ambao ni wazito katika ulipaji wa ada pia msisahau kuwaunga mkono wanawake wenzenu kutoka CCM ambao wanagombea nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi huu" .
Akiwa wilayani Kilombero aliwapokea na kuwakabidhi kadi mpya za CCM wanachama wawili ambao ni Zainab Henji na Sakina Stambuli kwa niaba ya wenzao 22 waliohama kutoka chama cha CUF.
Taasisi ya WAMA iliwachangia wanawake hao mchango wa Tshs. 500,000 kwa kila wilaya na Tshs. 200,000 kwa wanawake wa tarafa ya Malinyi fedha ambazo watazitumia katika shughuli za maendeleo .

You liked this post? Subscribe via RSS feed and get daily updates.

0 comments:

Post a Comment