MAJENGO YAJENGWA SHULE YA SEKONDARI MPANDA!!

Na Nkinda - Maelezo, Mpanda
30/10/2009 Serikali imetoa jumla ya Tshs. 52,000,000/= kwa ajili ya ujenzi wa madarasa manne, choo matundu sita na nyumba moja ya mwalimu katika shule ya Sekondari ya wasichana ya Mpanda.
Hayo yamesemwa jana na Mkuu wa shule hiyo Mwalimu Nyabise Sabasi wakati akitoa taarifa ya shule hiyo kwa Mke wa Rais Mama Salma Kikwete aliyetembelea shuleni hapo kwa ajili ya kuongea na wanafunzi wa kike wa wilaya ya Mpanda katika mkoa wa Rukwa.
Mwalimu Sabasi alisema kuwa katika utekelezaji wa ujenzi wa miradi hiyo shule imetoa mchango wake kwa kufyatua matofali laki moja na thelathini elfu. Pia shule iliandaa harambee kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa elimu ambapo zilipatikana Tshs.4,549,000/= ila bado kuna upungufu wa Tshs. 25, 595,145/= ili ujenzi wa miradi hiyo uweze kukamilika.
Shule hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na upungufu wa mabweni manne kwani shule hiyo ilijengwa kwa ajili ya kulala wanafunzi 320 lakini hivi sasa kuna wanafunzi 640 kutokana na tatizo hilo shule inatumia baadhi ya vyumba vya madarasa kuwa mabweni.
Aliendelea kuzitaja changamoto zingine kuwa ni ongezeko la wanafunzi yatima na wanaotoka katika mazingira magumu kwani hivi sasa shule hiyo ina wanafunzi 33 ambao hupata shida mbalimbali na kukosa mahitaji muhimu, baadhi yao hulazimika kubaki shuleni kwa vipindi vyote vya likizo lakini kuna wengine wanaacha shule kwa sababu ya maisha duni na wengine hulazimika kuingia kwenye vitendo viovu wakidhani kuwa watapata mahitaji muhimu kwa maisha.
"Tunakabiliwa na upungufu wa madarasa matatu,, upungufu wa nyumba za wafanyakazi, upungufu wa vitendea kazi vinavyoendana na karne ya sayansi na keknolojia, upungufu wa vitabu vya kidato cha tano na sita, ukosefu wa uzio, upungufu wa wafanyakazi na hatuna gari dogo ambalo litatumika wakati wa dharula", alisema.
Akiongea na wanafunzi wa kike 1500 kutoka shule za sekondari 15 Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema kuwa sababu za kihistoria zilikuwa zikiwanyima watoto wa kike fursa ya kupata elimu ikilinganishwa na watoto wa kiume.

You liked this post? Subscribe via RSS feed and get daily updates.

0 comments:

Post a Comment