JESHI LA POLISI KUENDELEA KUTOA TUZO KWA ASKARI NA WANANCHI!!

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Said Mwema akimtunuku nishani heshima Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam William kutokana na mchango wake wa kushirikiana na Jeshi la polisi kukabiliana na masuala mbalimbali wakati wa sherehe za kuwatunuku nishani maafisa polisi, askari na raia (wafanyabiashara) waliotoa michango mbalimbali kulisaidia jeshi la polisi leo jijini Dar es salaam.
(Picha, Habari na Aron Msigwa- MAELEZO).

30/10/2009, Dar es salaam.
Jeshi la Polisi limesema kuwa litaendelea kutoa tuzo kwa askari , raia na wafanyabiashara wanaotoa michango mbalimbali na kushirikiana na Jeshi hilo katika kufanikisha vita dhidi ya vitendo vya uhalifu nchini.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es salaam na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Said Mwema wakati wa sherehe za kuwatunuku nishani maafisa polisi na askari walioshiriki katika oparesheni za kulinda amani nchi Comoro na raia wema (wafanyabiashara) waliotoa michango mbalimbali ili kuliwezesha Jeshi la polisi kutekeleza majukumu yake ipasavyo.
Amesema mpango huo wa utoaji tuzo kwa wafanyakazi bora wa jeshi la polisi, raia na wafanyabiashara wanaoshirikiana na Jeshi la Polisi unatokana na jeshi kutambua mchango mkubwa walioutoa na wanaoendelea kuutoa katika kuboresha utendaji kazi ndani ya jeshi.
Amefafanua kuwa Jeshi la Polisi litaendelea kuwathamini askari wake kwa kuwapa motisha ili kuhakikisha kuwa ulinzi na usalama ndani ya nchi unaimarishwa.
“Hata tukiwa na magari, tuwe na ndege ni lazima tuthamini askari wetu kuliko kitu kingine ili kuhakikisha ulinzi na usalama pamoja na maisha bora kwa kila mtanzania yanapatikana” amesema.
Ameongeza kuwa viongozi wa Jeshi wataendelea kukaa pamoja ili kuvipima, kuviibua na kuviendeleza vithaminiwa vya polisi pamoja na kutoa zawadi kwa askari wanaofanya kazi nzuri ya kulinda mali na maisha ya raia ikiwa ni sehemu ya kuthamini mchango wao na kuwapa sifa stahiki.
Kuhusu Jeshi la Polisi kuendelea kushirikiana na raia wote katika Nyanja ya ulinzi shirikishi amesema kuwa Jeshi la Polisi linaandaa utaratibu ili kuhakikisha kuwa raia wote wanashiriki kikamilifu katika kujilinda wenyewe mahali wanakoishi pamoja na kuaandaa askari na maafisa wa polisi wa kudumu watakaoshirikiana na vikundi maalum vya ulinzi vitakavyoanzishwa katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es salaam.
Kwa upande askari waliotunukiwa nishani kwa kushiriki harakati za kulinda amani nchini Comoro Generali Mwema amesema ni mfano wa kuigwa kwani walifanya kazi katika nchi tofauti na waliyoiazoea pamoja na kushirikiana kikamilifu na askari kutoka katika nchini nyingine zilizoshiriki operesheni za ulinzi wa amani nchini Comoro.
Hata hivyo amesema Jeshi la Polisi liko makini kuhakikisha kuwa mafunzo ya askari yanaboreshwa ili kuwawezesha askari kufanya kazi kikamilifu watokapo mafunzoni hatua hii ikijumuisha mpango wa kuongeza mafunzo kivitendo zaidi kwa askari kwenye maeneo ya raia.
Mbali na hilo amesema Jeshi la Polisi linaendelea kufanya marekebisho kwa kuwawezesha kielimu askari wake ili kuwajengea uwezo na kulifanya kuwa la kisasa zaidi na lenye wataalam wa kutosha na hivyo kuongeza ufanisi katika majukumu ya kila siku.
Aidha ametoa wito kwa wananchi na kushirikiana na jeshi la Polisi katika kutimiza wajibu wake kwa ulinzi shirikishi na kuongeza kuwa mpango wa utoaji tuzo kwa wafanyakazi wa jeshi la polisi, raia na wafanyabiashara wanaoshirikiana na Jeshi la Polisi utaboresha mawasiliano na ushirikiano zaidi.

You liked this post? Subscribe via RSS feed and get daily updates.

0 comments:

Post a Comment