Na Anna Nkinda - Maelezo
08-09-2009 Arusha
Wawekezaji nchini wametakiwa kuwekeza katika viwanda vya kutengeneza nyuzi, nguo na kushona mavazi kwani kwa kufanya hivyo si kuwa wataongeza ajira na mapato ya nchi bali pia watawahakikishia wakulima wa zao la pamba masoko ya uhakika na bei nzuri ya zao hilo. Rai hiyo imetolewa leo na Rais Jakaya Mrisho Kikwete wakati akiongea na wananchi pamoja na wafanyakazi wa kiwanda cha kutengeneza nyuzi cha Jambo Spinning Mill kilichopo Usa River mkoani Arusha mara baada ya kufungua kiwanda hicho..
Rais Kikwete alisema kuwa kinachotakiwa hivi sasa ni kuongeza uzalishaji wa zao la pamba kwani kwa wastani wakulima wa hapa nchini wanazalisha kilo 200, 250 hadi kilo 300 wakati wakulima wa nchi za nje wanazalisha kilo 800 mpaka zaidi ya kilo 1000 kwa hekta.
"Sisi tunao uwezo wa kuzalisha pamba kwa wingi zaidi ya tunayoizalisha hivi sasa mara mbili hadi tatu kama tutaamua kwani bado hatujaanza kazi ya kuzalisha pamba hadi ikafika mahali tukajidai na hii ni moja ya shabaha kubwa ya serikali katika mkakati wa kusukuma kilimo kwa kasi kubwa zaidi ujulikanao kama kilimo kwanza", alisema.
Hivi sasa Serikali inaondoa vikwazo vya kuzuia uwekezaji hapa nchini inachofanya ni kuharakisha utoaji wa leseni, kuondoa urasimu katika masuala ya ulipaji wa kodi, kuwezesha viongozi na watendaji wa serikali kufanya maamuzi sahihi na kwa wakati muafaka na kuwezesha shughuli za uwekezaji kufanyika katika uwazi na kumalizika katika kituo kimoja.
Akisoma taarifa ya kiwanda hicho Salum Hamis Salum ambaye ni Mkurugenzi alisema kuwa nyuzi zinazotengenezwa katika kiwanda hicho zinatokana na pamba ya hapa nchini inayochambuliwa na kiwanda tanzu na hicho cha Jambo Ginnerry kilichopo mkoani Shinyanga.
Salum aliendelea kusema kuwa matarajio ya kiwanda hicho ni kufikia uwezo wa kufuma nguo za kisasa, kwa matumizi ya ndani na nje ya nchi huku wakiwa na lengo la kuingia katika soko la AGOA.
"Changamoto zinazotukabili ni kuyumba kwa uchumi wa Dunia ambako kwa kiasi kikubwa kumeathiri sana soko la nyuzi na gharama kubwa za uendeshaji wa kiwanda ikiwa ni pamoja na kupanda kwa gharama za umeme", alisema.
Mwaka 2004 watanzania wanaomiliki kiwanda hicho walianza uwekezaji wa zaidi ya dola za kimarekani milioni 50 katika ujenzi. Matarajio yao ni kukipanua zaidi kwa kuongeza uwekezaji hadi kufikia dola za kimarekani milioni mia mbili.
Hivi sasa kiwanda hicho kimeajiri wafanyakazi 220 na wanatarajia kutoa ajira kwa wafanyakazi 1000 kadri kinavozidi kupanuka.
Mwisho.





0 comments:
Post a Comment