Twanga Pepeta 'Kusugua Kisigino' Kiwalani, wamo Mrisho Mpoto na Wabogojo!!

Wanamuziki wa Bendi ya African Stars wakiwa wammejipumzisha katika moja ya kazi zao za kurekodi video zao.
BENDI ya muziki wa dansi ya African Stars 'Twanga Pepeta International' inatarajia kuwapa mashabiki wake wa Kiwalani, Dar es Salaam, burudani ya staili yake mpya iliyoshika kasi ya 'Sugua Kisigino' kwenye ukumbi wa Gaza Strip. Mkurugenzi wa Kampuni ya First Entertainment iliyoandaa onyesho hilo,
Victorian Nachenga 'Victor Buguruni', alisema Dar es Salaam jana kuwa bendi hiyo itafanya onyesho hilo Alhamisi (Julai 30, mwaka huu) kuanzia saa 3 usiku kwa kiingilio cha sh. 5,000. Victorian alisema Twanga Pepeta itasugua kisigino kwa wakazi wa Kiwalani na vitongoji vyake, onyesho ambalo pia ni sehemu ya kuendelea kutambulisha albamu ya 10 ya bendi hiyo, Mwana Dar es Salaam iliyozinduliwa mwezi uliopita kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee.
Alisema onyesho hilo pia litapambwa na burudani kutoka kwa wasanii wengine wakiwamo Mrisho Mpoto 'Mjomba', Athuman Ford 'Wabogojo', Steve Nyerere na Sunche na Kapeto. Mkurugenzi huyo alisema katika onyesho hilo maalumu, bendi hiyo itatambulisha nyimbo zake saba mpya zikiwamo Sumu ya Mapenzi uliotungwa na Khalid Chuma 'Chokoraa', Mwisho wa ubaya ni aibu (Saulo John 'Ferguson'), Sintopenda tena (Saleh Kupaza), Nazi haivunji jiwe. Nyingine ni Shida Darasa na Mwana Dar es Salaam uliobeba jina la albamu, zilizotungwa na Charles Gabriel 'Chalz Baba' na mwingine uliotungwa na Rogart Hega 'Katapila'.
Albamu nyingine ambazo bendi hiyo imewahi kutoa na kutamba katika anga za muziki nchini ni Kisa cha Mpemba mwaka 1999, Jirani (2000), Fainali uzeeni (2001), Chuki binafsi (2002), Ukubwa jiwe (2003), Mtu pesa (2004), Safari 2005 (2005) na Password (2006).

You liked this post? Subscribe via RSS feed and get daily updates.

0 comments:

Post a Comment