Jumla ya wanafunzi 623 wa kike katika Mkoa wa Kagera wapata Mimba!!

Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akiongea na wanafunzi katika moja ya ziara zake ambazo amekuwa akizifanya katika mikoa mbalimbali, hivi sasa yuko Mkoani Kagera kwa ziara ya siku tatu aliyoianza jana.

Na Anna Nkinda - Maelezo
26/07/2009 Kagera. Jumla ya wanafunzi 623 wa kike katika shule za Msingi na Sekondari mkoani Kagera wameacha shule kwa kipindi cha miaka miwili baada ya kupata ujauzito.
Hayo yamesemwa jana na Afisa elimu wa mkoa huo Florian Kimolo wakati akisoma tarifa ya maendeleo ya elimu kwa Mke wa Rais Mama Salma Kikwete ambaye ameanza ziara ya kikazi ya siku mbili mkoani humo.
Akifafanua taarifa hiyo Afisa elimu huyo alisema kuwa wanafunzi waliopata ujauzito wa shule ya Msingi ni 395 na wa Sekondari ni 228.
"Tatizo la mimba mashuleni limekuwa ni sugu katika mkoa huu kwani wanafunzi wengi wenye umri mdogo wamekuwa wakikatiza masomo yao kwa kupata ujauzito na hivyo kuharibu mwelekeo wa maisha yao", alisema Kimolo.
Aliendelea kusema kuwa wilaya ya Chato ndiyo inayoongoza kwa wanafunzi wengi kupata ujauzito kwani wanafunzi wa shule za msingi 130 na wa Sekondari 74 walipata ujauzito.
Ili kutatua tatizo hilo Serikali imewachulia hatua mbalimbali wahusika wa matukio hayo ambapo hadi sasa kuna kesi zinazoendelea kwa watendaji, mahakamani na Polisi pia watuhumiwa watano wamefungwa.
Naye Mama Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema kuwa muitikio wa elimu katika mkoa huo ni mkubwa wanachotakiwa kufanya ni kuzungumza na watoto pamoja na wazazi na kuonyesha ushirikiano wa hali ya juu lazima tatizo hilo litatatuliwa.
"Katika mkoa wa Kilimanjaro tatizo la upatikanaji wa mimba mashuleni lipo chini ukilinganisha na mikoa mingine hapa nchini ni vyema mkawauliza mbinu gani wamezitumia katika hilo na kuweza kufanikiwa ili nanti muende kujifunza", alisema.
Mama Kikwete ameanza jana ziara ya kikazi ya siku tatu katika mkoa wa Kagera yenye lengo la kuchangia juhudi za kupunguza vifo vya kinamama vinavyotokana na uzazi kwa kutoa vifaa vya huduma ya afya ya uzazi, hususan katika wodi za wazazi. Kuhamasisha juhudi za maendeleo kwa wanawake kupitia vikundi vya SACCOS na benki za vijijini- VICOBA.
Kuhamasisha juhudi za kupunguza matukio ya mimba na utoro mashuleni, kuhamasisha vikundi vya SACCOS na benki za vijijini- VICOBA na kuhamasisha juhudi za kupunguza matukio ya mimba na utoro mashuleni.

You liked this post? Subscribe via RSS feed and get daily updates.

0 comments:

Post a Comment