Wakenya wawang'oa Wanigeria Zain Africa Challenge!!

Dar es Salaam, Jumanne, Aprili 21, 2009
Chuo Kikuu cha Egerton kutoka Kenya juzi kiliibuka na ushindi dhidi
ya Chuo Kikuu cha Abubakar Tawafa Balewa kutoka Nigeria katika mechi ya saba ya mashindano ya chemsha bongo ya Zain Africa Challenge (ZAC)
yanayoendelea jijini Kampala, Uganda.
Chuo Kikuu cha Egerton ambacho ndio mabingwa watetezi baada ya kutwaa kombe mara mbili mfululizo, kiliwasambaratisha wapinzani wao Chuo Kikuu
cha Abubakar Tawafa Balewa, kwa kuwachapa kwa pointi 740 dhidi ya 570.
Wawakilishi wengine wa Tanzania, Chuo Kikuu cha Kumbukumbu cha Hubert Kairuki leo (Jumatano ya Aprili 22, 2009) wanatarajiwa kupimana ubongo na Chuo Kikuu cha Busoga kutoka Uganda, mchuano utakaooneshwa katika televisheni ya ITV saa tatu usiku.
Tanzania sasa inawakilishwa na vyuo vikuu vinne ambavyo ni Chuo Kikuu cha Kumbukumbu cha Hubert Kairuki, Chuo Kikuu cha Tiba na Sayansi Muhimbili, Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Tiba, Chuo Kikuu cha Mzumbe na Teknolojia (IMTU) baada ya Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (SAUT) kutolewa wiki iliyopita na Chuo Kikuu cha Lagos cha Nigeria katika mechi ya tano.
Mashindano ya ZAC yanaendeshwa kwa siku 31 katika mtindo wa mtoano na
yanashirikisha vyuo vikuu 32 kutoka katika nchi nane za Afrika
zinazozungumza Kiingereza ambazo ni Sierra Leone, Ghana, Nigeria,
Uganda, Kenya, Tanzania, Zambia na Malawi.
Mpaka sasa, vyuo vikuu vilivyofuzu raundi ya pili ni Jomo Kenyatta, Egerton kutoka Kenya, Ibadan, Lagos (Nigeria), Mzumbe (Tanzania), Mbarara (Uganda) na Valley View (Ghana); ilhali vyuo vilivyoaga mashindano hayo ni Kwame Nkhuruma (Ghana), Chuo Kikuu cha Malawi (Malawi), Njala (Sierra Leone), SAUT (Tanzania), Copperbelt (Zambia) na Abubakar Tawafa Balewa (Nigeria).

You liked this post? Subscribe via RSS feed and get daily updates.

0 comments:

Post a Comment