Serikali yatoa onyo kwa makandarasi wazembe!!

Waziri wa Nishati na Madini William Ngeleja (katikati) akionyeshwa moja ya mashine ya kuzalisha umeme (haipo pichani) na John Mageni (aliyenyosha mkono) ambaye ni Meneja uzalishaji wa mradi wa umeme wa gesi wa Somanga – Kilwa. Kushoto kwa waziri Ngeleja ni Mkuu wa mkoa wa Lindi Mecky Sadick.
Waziri wa Nishati na Madini William Ngeleja (kushoto) akisikiliza hatua ya maendeleo ya mradi wa umeme wa gesi wa Somanga - Kilwa kutoka kwa John Mageni (aliyevaa shati la light blue) ambaye ni Meneja uzalishaji wa mradi huo. Aliyesimama katakati yao ni Mkuu wa mkoa wa Lindi Mecky Sadick.
Na Anna Nkinda - Maelezo
02/03/2009 Kilwa Serikali imetoa onyo kali kwa makandarasi wazembe wanaowasababishia wananchi wasipate huduma kwa wakati na kusema kuwa hawatavumiliwa tena na hatua kali dhidi yao zitachukuliwa ili kukomesha tabia hiyo.
Onyo hilo limetolewa (jana) juzi na Waziri wa Nishati na Madini William Ngeleja alipotembelea ujenzi wa mradi wa umeme wa gesi wa Somanga - Kilwa na kujionea jinsi unavyosuasua na kushindwa kuanza kutoa huduma kwa wananchi.
Akiongea kwa ukali na makandarasi wa mradi huo waziri Ngeleja alitoa muda wa siku ishirini na moja kwa kampuni ya D.B. Shapriya kukamilisha ujenzi wa uzio na barabara za ndani katika eneo la mradi.
Pia alitoa siku tisini kwa Kampuni ya RENCO SPA kukamilisha kazi ya kuunganisha bomba la gesi kutoka Songas Main Valve hadi kwenye mtambo.
Makampuni hayo yalitakiwa kukamilisha kazi yake mwaka 2007 jambo ambalo lingesababisha wananchi wa wilaya ya Kilwa kupata umeme kutoka katika mradi huo.
Aidha waziri Ngeleja aliwaomba radhi wananchi wa wilaya ya Kilwa kwa kuchelewa kuanza kwa maradi huo na kusema kuwa hiyo ni kutokana na sababu za kiufundi na kiusimamizi.
“Hivi sasa Serikali inafuatilia kwa karibu zaidi mradi huu ili uweze kukamilika na wananchi wapate huduma ya umeme kama wanavyopata wananchi wa maeneo mengine hapa nchini”, alisema.
Aliendelea kusema kuwa wamejifunza kutokana na tatizo hilo na kuahidi kuwa hapo mbeleni watakuwa makini zaidi ili miradi yote iweze kukamilika na kufanya kazi kwa wakati muafaka.
Akiongelea kuhusu jinsi ya kupitisha umeme huo katika mto Rufiji na kuupeleka katika wilaya za Mkuranga na Temeke waziri Ngeleja alisema kuwa taratibu za kupata mkandarasi zimeshakamilika wanachosubiri ni mtaalamu awajulishe njia sahihi ya kupitisha umeme huo katika daraja la Mkapa ambapo kazi hiyo iataanza mwezi wa nne mwaka huu.
Waziri Ngeleja pia aliahidi kushughulikia tatizo la Jenereta kwa wakazi wa wilaya ya Kilwa ambalo linaharibika mara kwa mara na hivyo kuwafanya wakazi hao kutokupata umeme wa uhakika ambapo ndani ya mwezi huu tatizo hilo litakuwa limepata ufumbuzi.
Endapo mradi huo utakamilika kabla ya kupitishwa kwa umeme katika mto Rufiji wananchi wa wilaya ya Kilwa wataanza kupata huduma ya umeme bila ya kusubiri upitishwe mto Rufiji kwanza.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mecky Sadick alimwambia waziri Ngeleja kuwa mradi huo ilibidi ukamilike April mwaka 2007 lakini haelewi kwanini hadi sasa mradi huo haujakamilika jambo linalosababisha wananchi wa wilaya ya Kilwa waendelee kuteseka kwa kutokupata umeme wa uhakika.
Mkuu huyo wa Mkoa alisema, “Jenereta linalotumika wilaya ya Kilwa ni bovu kwani haziwezi kupita siku tatu bila ya kukatika kwa umeme tunakuomba waziri mradi huu uweze kukamilika mapema ili wananchi wa Kilwa wasiendelee kuteseka kwa kukosa umeme”.
Wakiongea kwa nyakati tofauti viongozi wa makampuni ambayo yamesababisha kuchelewa kuanza kwa mradi huo wamesema kuwa tatizo lilikuwa ni fedha kwani walikuwa wanaidai serikali lakini kwa kuwa hivi sasa wameshalipwa madeni yao wanaahidi watakamilisha kazi zao haraka kutokana na maagizo waliyopewa na waziri.
Kukamilika kwa mradi huo kutawanufaisha wakazi wengi wa wilaya za Kilwa, Rufiji, Mkuranga na Temeke kwani mradi huo ni fidia kwa maeneo na wananchi walioathiriwa na miundombinu ya usafirishaji gesi asilia ya Songosongo kutoka kisiwa cha Songosongo hadi Dar es Salaam.

You liked this post? Subscribe via RSS feed and get daily updates.

0 comments:

Post a Comment