Wadau wa muziki wa kizazi kipya Bongofleva hapa nchini Kebby na Jerry ambao waliwahi kuwa mameneja wa mwanamuziki mkongwe na mwanzilishi wa muziki huo hapa nchini Joseph Mbilinyi aka Mr. II wamezungumzia wimbi la kuvunjika kwa makundi ya muziki huo ambayo yamekuwa yakianzisha na wasanii kadhaa hapa nchini.
Wakizungumza na Tovuti ya FULLSHANGWE Kebby na Jerry wamesema ni vigumu makundi hayo kudumu kwa muda mrefu kutokana na mfumo wanaoutumia katika kuunda makundi yao au kutokana na mambo ya kiutawala yanavyokwenda ndani ya makundi hayo kwani waliowengi hawajasoma na hata kama wakibahatika kusoma bado tatizo linakuwa kwamba huwezi kujiongoza mwenyewe kwa kila kitu kwani kuna watu wapo wana uzoefu wamesomea utawala na wanajua utawala wa makundi ya muziki jinsi unavyotakiwa kuwa.
Kebby anaongeza kuwa makundi mengi yanaundwa katika vijiwe vya kuvutia bangi, na katika kuunda msanii anaweza kujipachika tu cheo aidha kwa sababu ni mbabe au kwa kuwa ana kipaji cha kuimba kuliko wengine au pengine yeye anaonekana kuwa na mvuto zaidi kwa mashabiki wa kundi hilo basi anaamua kujipa cheo yeye kitu ambacho wanamuziki wengine katika kundi wanakubali lakini kwa shingo upande kwa sababu wanakuwa hawana njia ya kuzuia au kukataa
Anasema kundi lolote likitaka mafanikio ni vyema likawa na uongozi makini yaani likampata meneja makini ambaye anaweza kuwajibika vyema kwa kundi ikiwa ni pamoja na kutafuta masoko na kuandaa programu yote ya kundi, mwanamuziki au wanamuziki kwa kile wanachotarajia kukifanya kwa wakati uliopo na ujao lakini pia kusimamia kwa umakini jambo lolote linalofanyika kwa wakati huo kama vile kuingia mikataba ya maonyesho kujua kwamba kama kuna nyimbo mpya watarekodi studio gani, kufanya malipo na kama kuna safari za mwanamuziki kujua atasafiri vipi, yote haya akifanya kwa kushauriana na wanamuziki wake au mwanamuziki wake kwa kuzingatia taratibu za kiutawala.
Anatoa mfano kuwa yeye na mwezie Jerry wakati walipokuwa mameneja wa MR II walikuwa wakifanya kila kitu kwa utaratibu mzuri ambao ulikuwa unamfanya hata Mr II kupumzika vya kutosha anaongeza kuwa pia walikuwa wanahakikisha maslahi yake hayavurugwi lakini pia walikuwa na msimamo kwani walikuwa hawatumfichi kama akivurunda jukwaani "yaani akishuka tu tunampasha na hatuongei mpaka tukifika Hotelini" kitu kilichamfanya hata yeye awakubali kwasababu waulikuwa wanahakikisha mambo yanakwenda vizuri ili yeye afaidike na wao pia wafaidike.
Kebby anasema kwa mfano makundi kama Hardblaster ambalo Pr. J aka Red Carpert alijitenga na kuanza kufanya kazi kivyake. TMK wanaume Family ambalo Juma Nature alijitenga na kuanzisha Wanamume TMK Halisi, Nako2nako pia waligawanyika, East Coast lililokuwa likiongozwa na Crazy Gk, TipTop Connection iliyokuwa na wanamuziki kama MB Dog , Gheto Boys lilioongozwa na Afande Sele hatimaye nalo lilisambaratika na mengine mengi.
Anasema kwamba wanamuziki wengi ambao wameweza kumudu kuendesha mambo yao wameajiri mameneja utaratibu ambao uko ulimwenguni kote umewasaidia kutokuwa na mrundikano wa majukumu kitu kunachowapa unafuu katika kupanga mikakati yao ya kimaendeleo.
Lakini pia anamaliza kwa kuwasifu wanamuziki kama Banana Zorro na Lady Jay Dee ambao wameanzisha bendi zao na mambo yao yanakwenda vizuri jambo ambalo linawaangazia nuru ya mafaniko katika siku za usoni, Mwanamuziki Banana Zorro anamiriki Bendi inayoitwa B. Band na Lady Jay Dee anamiriki bendi yake inayoitwa Machozi Band
0 comments:
Post a Comment