Rais Jakaya Kikwete kuipamba THT Dar!!

Rais Jakaya Kikwete akizungumza na Wananchi katika moja ya majukumu yake ya Kitaifa


Kundi la THT likifanya vitu vyake katika mashindano ya kutafuta wanamitindo bora Afrika mashariki na kati kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee hivi karibuni kundi hilo litafanya sherehe ya kutimiza miaka mitatu toka liundwe hivi karibuni.


RAIS Jakaya Mrisho Kikwete anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye sherehe ya kutimiza miaka mitatu ya taasisi ya kukuza vipaji vya muziki ya Tanzania House of Talent (THT), imefahamika.
Rais Kikwete anatarajiwa kujumuika ya wasanii mahiri kama vile Judith Wambura Mbibo ‘Lady Jaydee’, Joseph Haule ‘Profesa Jay’, Lawrence Malima ‘Marlow’ na Rashid Abdallah ‘Chid Benz’ katika hafla hiyo itakayofanyika Jumatatu Ukumbi wa Karimjee, jijini Dar es Salaam.
Mbali ya wasanii hao wengine wanaotarajiwa kushiriki ni maklundi ya Wanaume TMK, Wanaume Halisi, Selemani Msindi ‘Afande Sele’, Florence Kasella ‘Dataz’, Banana Zorro, Mandojo, Mwasiti, Maunda Zorro na Hafsa Kazinja.
Hafla hiyo imedhaminiwa na Mfuko wa Kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom ambako pamoja na mambo mengine, THT itatumia nafasi hiyo kukuza mfuko wake kwa kuchagiwa kwa ajili ya kuendeleza vipaji.
THT iko katika mpango wa kununua vifaa vya kisasa kwa ajili ya kufundishia muziki ambavyo vitatumika katika kutoa elimu hivyo kuwasaidia vijana kuendeleza vema vipaji vyao.
Tayari THT imeanza kufanya hivyo kwa baadhi ya vijana chipukizi wanaoibukia vema kwenye muziki kwa kutoa chakula mara mbili kwa siku na posho na matumizi madogo.
Baadhi ya chipukizi hao ni vijana waliopatikana mitaani wakiwa hawana uwezo wa kujiendeleza, yatima ambao wameendelezwa vema na sasa wanakuja juu katika tasnia ya sanaa.
Endapo itafanikiwa, THT inataka kuwa moja ya kituo bora nchini kinachoweza kuibua vipaji lakini haiwezi kufanya hivyo peke yake bila msaada wa fedha, elimu ya kutosha nakadhalika.
Inaelezwa kwamba bila ya THT, vipaji vingi visingejulikana na kupotea kabisa kwenye medani ya muziki hivyo Mfuko wa kusaidia wa Vodacom imejitokeza kutaka kuendeleza gurudumu la maendeleo ya vipaji mbele kwa kuandaa chakula hafla hiyo ya chakula cha jioni.
THT ilianzishwa Januari 2006, iko Kinondoni na kwa sasa ina mpango wa kuongeza eneo lake, vifaa mbalimbali ili kutoa elimu ya muziki na kwa kujitosheleza

You liked this post? Subscribe via RSS feed and get daily updates.

0 comments:

Post a Comment