Wasanii wa kikundi cha Nyangaria Group Investment kutoka Mjini Mwanza wakitumbuiza wakati wa sherehe ya siku ya familia katika mgodi wa Barrick Bulyanhulu iliyofanyika jana mgodini hapo.
Meneja Mkuu wa mgodi wa Barrick Bulyanhulu Greg Walker akitolewa damu ambayo itatumika kwa wagonjwa wakati wa sherehe ya siku ya familia iliyofanyika jana mgodini hapo. Huku Dk. Ghuhen Mtaita ambaye ni Daktari mkuu wa mgodi huo (kulia) na Adrew Marko ambaye ni afisa mhamasishaji wa mpango wa taifa wa damu salama kanda ya ziwa (kushoto) wakiangalia jinsi damu hiyo inavyotoka.
Na Mwandishi wetu
21/12/2008 Bhulyanhulu, Kahama.Wafanyakazi wa mgodi wa Barrick Bulyanhulu pamoja na familia zao wamejitolea lita 67 za damu wakati wa sherehe ya siku ya familia iliyofanyika jana mgodini hapo.
Dk. Ghuhen Mtaita ambaye ni Daktari mkuu wa mgodi huo alisema kuwa waliamua mwaka huu katika siku ya familia wachangie damu ili itumike kusaidia kuokoa maisha ya wagonjwa mbalimbali waliopo hospitalini.
“Lengo lilikuwa ni kupata lita 100 za damu ingawa hatujatimiza lengo ila tunaamini kuwa katika miaka ijayo tutachangia kiasi kikubwa cha damu kwani hii ni kampeni mojawapo tuliyonayo”, alisema Dr. Mtaita.
Daktari huyo aliendelea kusema kuwa kwa kuwa hii ni mara ya kwanza katika migodi ya Barrick hapa nchini kwa wafanyakazi pamoja na familia zao kujitolea damu ikiwa ni sehemu mojawapo ya kusherehekea sikukuu hiyo hivyo basi wameamua kufanya zoezi hilo mara tatu au mara nne kwa mwaka.
Naye Adrew Marko ambaye ni afisa mhamasishaji wa mpango wa taifa wa damu salama kanda ya ziwa aliwashukuru wafanyakazi wa mgodi huo pamoja na familia zao kwa ushirikiano wao waliouonesha hasa katika kuchangia damu.
Aliendelea kusema kuwa damu waliyoipata ambayo itatumika kwa wagonjwa 201 inatosha kwani wanachotaka wao ni ubora wa damu na si wingi wa damu.
Damu hiyo ambayo itapelekwa katika kituo cha kuchangia damu salama cha kanda ya ziwa kilichopo karibu na hospitali ya rufaa ya Bugando jijini Mwanza, itatumika kwa wagonjwa ambao ni watoto walio chini ya umri wa miaka mitano, mama wajawazito ambao huhitaji damu kabla na baada ya kujifungua, ajali mbalimbali, upasuaji wa dharula na kwa wagonjwa wengine watakao hitaji damu.
Marko alisema, “Kazi yetu sisi ni kukusanya damu na kuipima kisha kuzitawanya na kuzigawa katika hospitali za mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Kagera na Mara pamoja na hospitali za wilaya za mikoa husika, hospitali za mashirika ya dini na hospitali za watu binafsi ambazo wameruhusiwa kuongeza wagonjwa damu chini ya mpango wa Taifa wa damu salama”.
Afisa huyo mhamasishaji alimalizia kwa kuwaomba watanzania kuwa na mazoea ya kuchangia damu mara kwa mara kwani mahitaji ya damu kwa wagonjwa ni makubwa na upatikanaji wake ni mdogo.
Aidha Meneja Mkuu wa mgodi huo Greg Walker alisema kuwa lengo la siku hiyo kuwakutanisha pamoja menejimenti ya mgodi, wafanyakazi pamoja na familia zao na kukaa pamoja ili kubadilishana mawazo kwani wote wanafanya kazi kwa lengo moja na wanashangilia mafanikio pamoja.
“Siku ya leo wafanyakazi wamepata nafasi ya kukaa pamoja na kula pamoja na familia zao pia watoto wamecheza michezo mbalimbali ambayo imewajenga kimwili na kiakili pia”, alisema Walker.
Lengo lingine la kuwa na sikukuu hiyo ni kujua kwa kipindi cha mwaka mzima ni mafanmikio gani waliyoyapata pamoja na matatizo waliyokumbana nayo na changamoto gani zinawakabili katika utendaji wao wa kazi za kila siku.
Katika kusherehekea siku hiyo ambayo inafanyika kila mwisho wa mwaka
familia zilipata nafasi ya kucheza michezo mbalimbali ikiwemo michezo ya kukimbia, kukimbiza kuku, kuogelea, kucheza muziki, kuvuta kamba, mashindano ya kula matunda ya apple na kuruka.
0 comments:
Post a Comment