kampeni ya JK ya upimaji wa ukimwi kwa hiari yafanikiwa kutoka watu milioni 2 hadi 6.8

Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Prof. David Mwakyusa akiongea katika moja ya mikutano aliyowahi kuzungumza na wadau mbalimbali wa Afya.

NA ZAWADI MSALLA NA MAGRETH KINABO – MAELEZO

IMEELEZWA kuwa ya idadi ya watu wanaopima virusi vya ugonjwa wa Ukimwi kwa hiari baada ya kuzinduliwa Kampeni ya Kitaifa ya Upimaji wa Virusi vya Ukimwi kwa hiari, imeongezeka kwa kiasi kikubwa, kutoka watu milioni 2,000,000 kipindi cha mwaka 2005 hadi kufikia watu milioni 6,836,450 mwaka huu.
Hayo yalisemwa na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Profesa David Mwakyusa wakati alipokuwaakiwasilisha taarifa ya mafanikio ya serikali ya awamu ya nne katika kipindi cha miaka mitatu na kuzungumza na waandishi wa habari jana kwenye ukumbi wa mikutano wa wizara hiyo, jijini Dar es Salaam.
“Ongezeko kubwa la waliopima kwa hiari virusi vya UKIMWI limetokana na Kampeni ya Kitaifa iliyozinduliwa na kuongozwa na Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete na mke wake Mama Salma Kikwete Julai 14, mwaka 2007,” alisema Profesa Mwakyusa.
Profesa Mwakyusa aliongeza kuwa katika kipindi cha Disemba 2005 hadi Disemba 2008, kumekuwa na ongezeko la huduma katika maeneo mbalimbali za kupambana na maambukizi ya virusi vya ukimwi.
Alisema idadi ya vituo vya upimaji wa Ukimwi kwa hiari vimeongezeka kutoka vituo 515 mwaka 2005 na kufikia vituo 1,643 mwaka huu.
Aliongeza kuwa idadi ya wagonjwa wapatiwa dawa za kurefusha maisha(ARVs) imepanda kutoka wagonjwa 23,951mwaka 2005 hadi wagonjwa 189,050 sambamba na kuonzeka kwa idadi ya vituo vinavyotoa huduma ya tiba na matunzo ambayo ilikuwa ni vituo 96 na kufikia vituo 400 katika kipindi hicho.
Alisema kutokana na mapambana hayo viwango vya maambukizi ya virusi vya ukimwi hapa nchini vimeshuka kutoka wastani wa asilimia 7 mwaka 2005 kufikia asilimia 4.8 mwaka 2008, kufuatia kampeni ya hiyo.
Waziri Mwakyusa alisema asilimia 34 ya wanawake wote wajawazito wenye maambukizi ya virusi vya Ukimwi walipata dawa za kuzuia maambukizi hayo yasiende kwa watoto wao na kuongeza kwamba idadi ya vituo vinavyotoa huduma ya kuzuia maambukizi ya virusi hivyo kutoka kwa mama mjamzito kwenda kwa mtoto vimeongezeka kufikia vituo 2,474 ukilinganisha na ile ya awali ya vituo 544 wakati wa kipindi hicho.
“Wizara imeandaa Mpango Mkakati mpya wa Kisekta wa Kudhibiti Ukimwi kwa kipindi cha miaka mitano 2008-2012. Mpango huo unalenga kuwezesha upatikanaji wa huduma muhimu za kudhibiti na kutibu Ukimwi nchini,” alisisitiza.
Wakati huohuo Waziri Mwakyusa alizungumzia kuhusu Huduma za Maabara na Ufundi wa Vifaa Tiba, ambapo alisema, maabara zote za Rufaa na Mikoa zimepewa mashine za kuchunguza damu na uwezo wa figo na ini pamoja na chembe chembe za kinga – CD4 kwa ajili ya uanzishwaji na ufuatiliaji wa matibabu ya wagonjwa wa Ukimwi.
Pia maabara zote za wilaya zimepewa mashine za kuchunguza damu na uwezo wa figo na ini kwa ajili ya ufuatiliaji wa matibabu ya wagonjwa wa Ukimwi na maabara zote za Kanda zimepewa mashine maalum (DNA PCR) kwa ajili ya kuchunguza maambukizi ya virusi vya Ukimwi (VVU) kwa watoto wachanga chini ya miezi 18.
“Utaratibu wa kitaifa wa upimaji wa haraka wa VVU (National HIV rapid testing algorithm umebadilishwa kutoka utaratibu wa ‘Capillus’ iliyohitaji kutunzwa kwenye ubaridi na kutumia utaratibu wa ‘SD Bioline usiyohitaji kutunzwa kwenye ubaridi,” alisema.

Kwa upande lishe na Ukimwi alisema watoa huduma majumbani 111 katika wilaya 37 za mikoa ya Kilimanjaro, Tanga, Arusha, Mbeya, Rukwa na Iringa wamepata mafunzo kuhusu lishe kwa wagonjwa wenye Ukimwi na nakala 17,000 za mwongozo wa kitaifa kuhusu lishe bora kwa watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi na wenye Ukimwi, zimechapishwa na kusambazwa kwenye hospitali, Vyuo vya Afya na taasisi mbalimbali zinazojihusisha na masuala ya ugonjwa huoI.
Alisema utafiti wa chakula kinachofaa kuongeza virutubishi vya vitamini na madini kwa ajili ya watu wanaoishi na virusi vya hivyo na wenye ugonjwa huo umefanyika ambapo tafiti hii imeonyesha chakula hiki ambacho kinatokana na mazao yanayopatikana hapa nchini yameonyesha uwezo wa kuboresha afya ya watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi na wenye Ukimwi .

Mwakyusa alisema chakula hicho kinatokana na mchanganyiko wa unga wa mahindi, soya pamoja na virutubishi vya madini na vitamini ambavyo vyote vinapatikana nchini,hivyo matokeo ya awali yameonyesha kuwa afya ya watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi na wenye Ukimwi waliotumia chakula cha namna hiyo imeimarika.

You liked this post? Subscribe via RSS feed and get daily updates.

0 comments:

Post a Comment