Utabiri wa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Samwel Sitta ni zaidi ya Pweza Paul ambaye amekuwa akisifika kote ulimwenguni kwa utabiri wake alioitabiria timu ya taifa ya Ujerumani katika michezo yake yote sita ya kombe la dunia lililomalizika nchini Afrika Kusini hivi juzi.
Nathubutu kusema hivi kutokana na utabiri wake Spika Sitta alioutoa katika mahojiano aliyoyatoa kwenye kituo cha redio Clouds kipindi cha Powerbreakfast kuhusu michuano hiyo ya kombe la Dunia kabla haijaanza, ambapo alisikika mara kwa mara katika mahojiano hayo akisema hivi. Namnukuu.
"Mimi ni shabiki mkubwa wa timu ya Brazil na naipenda sana lakini katika timu zote zinazoshiriki Kombe la dunia nchini Afrika Kusini naona Hispania ina nafasi ya kufanya vizuri kwa kuwa ni timu inayocheza kwa pamoja na kwa ufundi mkubwa, hivyo timu hiyo ni tishio na inaweza kufika mbali na huenda ikachukua kombe la Dunia"
Haya yalikuwa ndiyo maneno ya Spika Sitta katika mahojiano hayo kabla ya kuanza kwa michuano hiyo na baada ya kuanza na kila siku ujumbe huu ulikuwa ukirudiwa kutangazwa kwenye kituo cha hicho kipindi cha Powerbreakfast.
Jambo hili halikunishangaza hata kidogo kwani kwa binadamu yeyote anayelijua jambo vizuri anaweza kulichambua kwa uhakika zaidi na ukawa ukweli kama ilivyotokea kwa timu hii ya Hispania kutoka bara la Ulaya kuchukua Kombe hilo wakati ilipoifunga timu ya Uholanzi goli 1-0 kwenye mchezo wa fainali uliochezwa kwa dakika 120 baada ya kutoka sare ya bila kufungana katika dakika 90 za mwanzo na kuongezwa dakika 30 kwenye uwanja wa Soccercity jijini Johanesburg.
Hata hivyo binadamu tunatakiwa kuamini zaidi katika kile ambacho binadamu mwenzio anaweza kukiangalia na kukichambua kiakili katika kujua ubora wake na udhaifu wake kama alivyofanya Mh. Samweli Sitta kwani ili kuichambua soka unahitaji kujua vitu vingi muhimu kuhusu mchezo huo.
Hongera sana Mh Samwel Sitta kwani ulitabiri kabla ya kuanza kwa michuano hiyo na imedhihirika kwamba utabiri wako ulikuwa ni wa kweli na umeonyesha kuwa una uwezo mkubwa wa kufuatilia mpira wa miguu na kujua ubora wa timu na udhaifu pia kwani ulisema wazi kwamba unaipenda Brazil lakini hukuonyesha mapenzi yako kwa timu hiyo ila ulisema ukweli unaoujua kwa kila timu iliyoshiriki kwenye michuano hiyo ya Kombe la Dunia.






1 comments:
Uhispania iliifunga Ujerumani katika fainali za Euro 2008 na si Uholanzi
Post a Comment