Wakenya watakiwa kuchangamkia soko la pamoja la Afrika mashariki!!


Na Anna Nkinda - Nairobi


Wakenya wametakiwa kuchangamkia mkataba wa soko la pamoja la Jumuia ya Afrika ya Mashariki ambao utawawezesha kufanya biashara, kazi na kuishi mahali popote wapendako ndani ya nchi wanachama, kupata fursa nzuri ya kuchuma mali zaidi na hivyo kujikwamua na maisha ya umaskini.


Wito huo umetolewa jana na Rais wa Nchi hiyo Mwai Kibaki wakati akiwahutubia wananchi kwenye maadhimisho ya miaka 47 ya sherehe za sikukuu ya madaraka iliyofanyika katika uwanja wa Nyayo jijini Nairobi.

Kibaki alisema kuwa mkataba huo ambao utasainiwa mwezi wa saba mwaka huu utatoa fursa nzuri ya kuchuma mali zaidi kwa wananchi wa nchi za Afrika Mashariki, kubuni nafasi za kazi na kuondoa umaskini.

“Katika ngazi ya kanda hii , ni fursa yangu kuona kwamba mkataba wa soko la pamoja la Jumuia ya Afrika mashariki utaanza kutekelezwa hivi karibuni hivyo basi Serikali yangu inashirikiana kikamilifu na nchi wanachama wa jumuia hii kuhakikisha kuwa utendaji kazi wa vipengele vyote vya mkataba huu unakamilika”, alisema Kibaki.

Kibaki pia alitoa rai kwa wakenya kuwakaribisha kaka na dada zao kutoka nchi za Uganda, Tanzania, Burundi na Rwanda ambao nao wataingia katika nchi hiyo kujitafutia riziki na kusema kuwa hiyo ndio njia ya kuonyesha shukrani na moyo kwa Jumuia ya Afrika Mashariki.
Aliendelea kusema kuwa hivi sasa wanapenda kufungua kabisa eneo la kaskazini Kenya na kustawisha uhusiano wa kibiashara na uwekezaji na majirani zao.

Serikali ya nchi hiyo hivi karibuni ilitoa kandarasi za kufanya uchunguzi wa ujenzi wa bandari ya Lamu, ujenzi wa reli kutoka Lamu kupitia Isiolo hadi Juba na kutoka Lamu-Isiolo hado Moyale.

Kibaki alisema “Ujenzi wa vifaa hivi vya muundombinu msingi utaanza hivi karibuni. Vilevile tumetoa zabuni ya kujenga reli ya kisasa kutoka Mombasa hadi Malaba na pia tutaimarisha zaidi huduma ya uchukuzi wa abiria kupitia magari ya moshi hapa jijini Nairobi”.

Kibaki alisema, “Matukia haya yakijumuishwa na uwekezaji tunaoufanya katika upanuzi wa barabara, utoaji wa nguvu za umeme, huduma za maji, huduma za simu na viwanja vya ndege ni ishara ya kutosha kwamba tunatayarisha nchi hii kwa hatua ya ubunifu wa nafasi za kazi na ustawi chini ya ruwaza ya maendeleo ifikapo mwaka 2030”.

Alifafanua kuwa ndiyo sababu hivi sasa wanaharakisha kazi za ujenzi wa barabara kuu ya Nauru - Eldoret hadi Malaba na kutoka Kericho hadi Kisumu na vile vile kupanua uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kisumu ili kuhakikisha uchukuzi bora wa watu na ushiriki wa haraka wa masoko unafanyika.

Kuhusiana na uchumi wa nchi hiyo Mwaikibaki alisema kuwa mwaka jana uliimarika kwa asilimia 2.6 kutoka asilimia 1.6. Kwa mwaka huu unatarajiwa kukuwa zaidi kati ya asilimia 4 na 5 . Hii ni kwasababu wakenya hata wakati wa hali ngumu, wanaendelea kufanya kazi kwa bidii kuimarisha maslahi yao binafsi na ya nchi.


Naye waziri Mkuu wa Nchi hiyo Raila Odinga alisema kuwa wakenya kabla ya kupata uhuru walikuwa wananyanyaswa sana na mabepari wa kikoloni ambao walikataa kuwapa uhuru wao kwa madai kwamba hawawezi kujitawala.


“Hivi sasa tuko huru tunahitaji kuwa na katiba yetu wenyewe kwani katiba tunayoitumia sasa ilitungwa na wakoloni huko katika nyumba ya Lang’ata hakuna hata mkenya mmoja aliyeshiriki, baada ya miaka mingi tumeona ni vyema tuwe na katiba yetu wenyewe lakini bado kuna watu wanaopinga kama vile wakoloni walivyopinga kutupatia uhuru wetu”, alisema Odinga.

Aliwaomba wananchi waliojiandikisha kupiga kura wajitokeze kwa wingi kupiga kura ya ndiyo tarehe nne Mwezi wa nane mwaka huu wakati wa kura ya maoni ili wakenya wapate katiba mpya waliyoiandaa wenyewe.

Kenya ilipata uhuru wake mwaka 1963 baada va mapigano yaliyosababisha watu wengi kupoteza maisha yao kutoka kwa wakoloni wa kiingereza.

You liked this post? Subscribe via RSS feed and get daily updates.

0 comments:

Post a Comment