SERIKALI KUBORESHA HUDUMA YA UTOAJI MAJI KWA WAKAZI WA JIJI LA DAR ES SALAAM!!


(Na Veronica Kazimoto - MAELEZO)

Jumla ya shilingi bilioni moja zitatumika katika kuboresha huduma za maji na kuongeza visima ili kuondoa kero za maji zinazowakabili wananchi wa maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam William Lukuvi amesema huduma hii imeanza kutekelezwa kuanzia sasa hadi mwezi Septemba mwaka huu na amesisitiza kuwa fedha hizo zimetoka Wizara ya Maji na Umwagiliaji, DAWASCO, DAWASA, Manispaa ya Kinondoni na Manispaa ya Temeke.

Lukuvi amesema kati ya fedha hizo, jumla ya shilingi milioni mia nane thelathini na tano elfu zitatumika kuchimba visima kumi na nane ambapo visima 8 vitachimbwa katika maeneo ya Kimara, Mburahati 2, Chang’ombe 3, Keko 3 na Sandari 2.

“Kiasi cha shilingi milioni mia sita na ishirini zitatumika kuunganisha mtandao wa mabomba mapya ya maji katika maeneo yaliyorukwa ambayo ni Ubungo – Kimara, Makuburi, na Tabata kwa ujumla”. Amesisitiza Lukuvi.

Lukuvi amefafanua kuwa fedha zingine zitatumika kuboresha mgao wa maji, kupitia upya utaratibu wa usambazaji na kutoa ratiba ya uhakika ya mgao wa maji ili kuongeza uwiano wa upatikanaji wa huduma ya maji pamoja na kudhibiti bei za maji katika Vioski vya maji, Mikokoteni na Maroli yanayouza maji kiholela.

Hata hivyo mkuu wa mkoa amesema bei ya kuuza maji kwenye vioski vya maji, maroli na wote wanaofanya biashara hiyo itasimamiwa na EWURA na bei rasmi ya maji kwa lita ishirini itatangazwa kabla ya mwisho wa mwezi huu.

Hatua hii imetokana na ziara ya Rais Jakaya Kikwete iliyofanyika mwezi Mei mwaka huu katika maeneo ya Mburahati, Kimara na Chang’ombe ambapo alikagua shughuli za utoaji wa huduma za maji safi na maji taka jijini Dar es Salaam.

You liked this post? Subscribe via RSS feed and get daily updates.

0 comments:

Post a Comment