Na Mohammed Mhina, wa Jeshi la Polisi
Wananchi wa Mikoa ya Kusini mwa Tanzania wameiomba Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya ndani kuangalia upya vigezo vya ajira kwa Jeshi la Polisi vinavyozingatia urefu ili kutoa nafasi kwa vijana wasio na sifa hizo kunufaika na ajira kwenye Jeshi la Polisi.
Wananchi hao wametoa ombi hilo kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Inspekta Jenerali Saidi Mwema, wakati wa ziara yake ya wiki moja mkoani Ruvuma ambapo wamesema kuwa kufuatia kigezo cha urefu, kimewafanya vijana wengi wa Mikoa hiyo kukosa nafasi ya kuajiriwa kwenye chombo hicho hata kama wanaviwango vikubwa vya ulemu na ujuzi mbalimbali.
Akizungumza katika mkutano huo, mkazi mmoja wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma Bw. Joseph Mapunda, amesema kuwa, kwa muda mrefu sasa, vijana wa mikoa ya Ruvuma, Mtwara na Lindi ambao wengi wao ni wafupi wakilinganishwa na vijana wa mikoa mingine hapa nchini, wamekuwa wakikosa nafasi za ajira katika Jeshi hilo na Majeshi mengine kutokana na maumbile yao.
Amesema baadhi ya vijana waliokuwa wakiomba kujiunga na majeshi ya ulinzi na usalama hapa nchini wamekuwa wakiambulia patupu kutokana na kikwazo hicho pamoja na kwamba wana nia na ari ya kulitumikia taifa lao ndani ya Majeshi hayo. Hata hivyo IGP Mwema, amesema nia ya Jeshi la Polisi ni kuajiri askari kutoka katika kila wilaya na mikoa hapa nchini kwa lengo la kuwa na Jeshi lenye sura ya Kiataifa na kwamba kigezo cha urefu kitatazamwa upya hasa kwa baadhi ya vijana wa maeneo ya mikoa ya kusini mwa Tanzania.
Amesema kwa kufanya hivyo, kutatoa fursa kwa vijana wengi wa Kitanzania wenye elimu inayotajwa kwenye sifa za ajira katika majeshi yetu kuweza kujiunga. Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Jeshi la Polisi nchini ametoa wito kwa Watanzania kutumia haki yao ya Kikatiba katika uchaguzi Mkuu ujao baadaye Oktoba mwaka huu kwa kuwachagua viongozi wanaodhani kuwa wataliongoza taifa letu kwa amani na utulivu.
IGP Mwema alikuwa akizungumza katika mikutano tofauti huku akinadi katika wilaya alizozitembelea mkoani Ruvuma na huku akinadi kitabu cha wajibu wa mpiga kura kilichoandaliwa na Jeshi la Polisi nchini kama dira kwa Watanzania kuelekea uchaguzi mkuu ujao hapo baadaye mwaka huu.
0 comments:
Post a Comment