WATOTO WA "MO" KUIKABILI KAGERA SUGAR JUMAMOSI UWANJA WA KAITABA!!

Mbunge wa Singida Mjini na mmiliki wa timu ya Africa Lyon Mohammed Dewji akishuhudia moja ya mchezo wa mpira wa miguu kwenye uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaam.

Timu ya Africa Lyon ya jijini dar es salaam tayari imeondoka kuelekea mkoani kagera kwa ajili ya pambano lao la ligi kuu ya Vodacom litakalofanyika kati yake na timu ya Kagera Sugar ya huko katika uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba siku ya Jumamosi.
Akizungumzia safari hiyo msemaji wa timu hiyo Kambi Mbwana amesema timu imeondoka na wachezaji wakiwa na ari ya ushindi ili kujiimarisha zaidi na kuondokana na kabisa na ishara ya kushuka daraja katika msimamo wa ligi hiyo na ameongeza kuwa timu inakwenda Kagera ili kurudi na paointi tatu na si vinginevyo.
Kwa sasa Africa Lyon ina pointi 19 mara baada ya kutoka sare na timu ya Simba kwenye mchezo uliochezwa kwenye uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaam hivi karibuni na ni ya sita katika msimamo wa ligi ya Vodacom.
Hivyo timu hiyo inayomilikiwa na mwanamichezo kabambe na Mbunge wa jimbo la Singida mjini Mohammed Dewji ama "MO" kama wanavyopenda kumwita inapigania kupata pointi zingine tatu ili iweze kufikisha pointi 22 na kujihakikishia kubaki katika kapu la timu zinazoshiriki ligi kuu ya Vodacom ambayo hivi sasa inaelekea ukingoni.
Simba ndiyo inayoongoza Ligi hiyo ikiwa na pointi 52 wakati Yanga ambao ni mabingwa watetezi wanafuatia kwa kuwa na pointi 42.

You liked this post? Subscribe via RSS feed and get daily updates.

0 comments:

Post a Comment