SERIKALI YAWATAHADHALISHA WAFANYABISHARA WA MADINI JUU YA KUZUKA KWA WIMBI LA MATAPELI.


Na Veronica Kazimoto – MAELEZO Dar es Salaam
Kamishna wa madini nchini Tanzania kutoka Wizara ya Nishati na Madini Dkt. Dalaly Kafumu amewatahadhalisha wananchi wote wakiwemo raia wa kigeni kuwa kumezuka wimbi la utapeli katika bishara ya madini hasa ya dhahabu na almasi.
Akizungumza jijini Dar es salaam leo, Dkt Kafumu amesema matapeli hao wanatoka nchini Tanzania na nchi ya jirani ya Jamhuri ya kidmokrasia Kongo ambao wamekuwa wakiwatapeli wananchi na raia wa kigeni kwa kuwasiliana nao kwa kutumia barua pepe wakiwapa taarifa za uongo za kuwavutia waje nchini kununua madini kwa bei nafuu.
Dkt kafumu ameeleza kuwa matapeli hao huwasiliana na wafanya biashara wa nje na huwapa majina ya kampuni hewa ambazo zinamiliki kiasi kikubwa cha dhahabu au almasi na huuza madini hayo kwa bei nafuu.
“Wafanyabuashara wengi wa kigeni hutumbukia kwenye mitengo ya matapeli hao kwa kuvutiwa na bei ndogo ya madini na kuja nchini wakitegemea kupata faida kubwa watakapouza madini hayo nje ya nchi.” Amesema Dkt Kafumu.
Dkt kifumu amesisitiza kuwa wafanyabiashara wa kigeni wanapokuja nchini kununua madini hayo, matapeli huwaonesha masanduku yaliyojaa dhahabu au almasi bandia pamoja na taarifa za maabara zinazoonesha kuwa dhahabu hiyo imechunguzwa na kugundulika kuwa na ubora wa hali ya juu.
Aidha Matapeli hao huoneshwa nyaraka bandia zilizogongwa mihuri ya Serikali na Idara ya Forodha zikionesha kiasi cha dhahabu na thamani yake kitu kinachowafanya wafanyabiashara hao waamini kuwa madini hayo ni halali.
Hata hivyo Dkt kafumu amewashauri wafanyabishara wa madini wafike au kutoa taarifa kwenye ofisi za madini ili kupewa mwongozo kuhusu taratibu za kufanya biashara hiyo kabla ya kuingia mkataba na kampuni yoyote. Vilevile wafanyabiashara hao wakikumbana na vitendo vya utapeli watoe taarifa jeshi la polisi ili hatua za kisheria zichukuliwe haraka.

You liked this post? Subscribe via RSS feed and get daily updates.

0 comments:

Post a Comment