Na Ally Changwila- Ofisa wa Habari Wizara ya Maji na Umwagiliaji.
Waziri wa Maji na Umwagiliaji Profesa Mark Mwandosya ameuagiza uongozi wa Chuo cha Maendeleo ya Usimamizi wa Maji kukamilisha mchakato wa kuwa chuo kikuu ifikapo Mei mwaka huu.Profesa Mwandosya alitaka mchakato huo ukamilike mapema ili chuo hicho kianze kuchukua wanachuo katika ngazi hiyo ifikapo mwezi Septemba mwaka huu.
Waziri Mwandosya ameyasema hayo jana alipofanya ziara ya siku moja katika chuo hicho ambacho awali kilikuwa chini ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji lakini kwa sasa kipo katika hatua za kuwa wakala kamili tangu Agosti mwaka 2008, ili kujionea hali ya chuo hicho ikiwemo kuzungumza na wanafunzi, walimu na wafanyakazi wengine.Waziri Mwandosya alisema kwa uzoefu wake katika vyuo mbalilmbali alivyowahi kusoma na hata kufundisha , hali aliyojionea katika chuo hicho ni nzuri, japo haina maana kwamba chuo hicho hakiitaji kuboreshwa zaidi.“ Umuhimu wa chuo hiki ni mkubwa na lengo la wizara yangu ni kukifanya kiwe chuo bora kinachotoa wataalam wa masuala ya maji hata kwa nchi zingine,’”alisema Profesa Mwandosya.
Profesa Mwandosya ali kuongeza kuwa ameelezwa juu ya matatizo ya upungufu wa wataalam, nyenzo za kufundishia ikiwemo masuala ya Teknohama, usafiri katika chuo hicho ,hivyo aliahaidi kuwa hayo yote pamoja na ukarabati wa majengo yatatekelezwa katika mpango wa Programu ya Maendeleo ya Maji(WSDP) ya mwaka 2006-2015 inayotekelezwa na wizara yake.Awali alipokea maswali na maoni mbali mbali kutoka kwa walimu,wafanyakazi na Wanafunzi na kuongeza kuwa karibu yote yaliyozungumzwa akiondoa ile alama ya kuuliza yanabakia kuwa ni ushauri tu ambao ameuchukua na kuahidi kuufanyia kazi japo sehemu kubwa tayari imeshafanyiwa kazi katika mpango wa WSDP.Naye Mkuu wa Maabara ya Maji chuoni hapo, Victoria Kazinje alisema maabara hiyo ni chachu ya maendeleo ya sekta ya maji kwani imetoa wataalam wengi wenye ubora ambao wako sehemu mbalimbali nchini.
Kwa upande wake Waziri Mwandosya akizungumzia kuhusu maabara hiyo, aliwaagiza wahusika chuo hicho, kuhakikisha wanafuatilia hatua za kuhakikisha kazi zinazofanywa na maabara hiyo zinatambulika kisheria.






0 comments:
Post a Comment