Precision Air yasaidia waathirika wa mafuriko Kilosa!

Mkurugenzi Mtendaji na Ofisa Mtendaji Mkuu, Alfonse Kioko wa Kampuni ya ndege ya Precision Air, Alfonse Kioko (kulia), akimkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Halima Dendego, msaada wa saruji mifuko 200 na mabati 200 vyenye thamani ya sh. milioni 5.4, kusaidia ujenzi wa nyumba za walioathirika kwa mafuriko wilayani humo. Hafla hiyo ilifanyika juzi mjini Kilosa.
Na Mwandishi Wetu, Kilosa
KAMPUNI ya ndege ya Precision Air imetoa msaada wa mifuko 200 ya saruji na mabati 200 vyenye thamani ya sh. milioni 5.4 kwa waathirika wa mafuriko wilayani Kilosa.
Msaada huo ulioambatanana na fulana na kofia, ulitolewa mjini Kilosa juzi (Machi 10, 2010) huku Mkurugenzi Mtendaji na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Precision Air, Alfonse Kioko akikabidhi kwa Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Halima Dendego.
Ujumbe wa viongozi na wafanyakazi wa Precision Air ukiongozwa na Kioko ulikwenda mjini Kilosa juzi kuwafariji waathirika hao, na Dendego aliwashukuru kwa msaada huo.
"Precision imetoa mfuko 200 ya saruji na mabati 200 ikiwa ni pole kwa waathirika, kuitikia mwito wa Rais Jakaya Kikwete kuwasaidia waathirika wa mafuriko... tunatoa mwito kwa kampuni na mashirika mengine kujitokeza kuwasaidia," alisema Kioko.
Mkuu wa wilaya huyo alisema msaada huo utatumika kuwajengea nyumba za kudumu waathirika hao katika eneo maalumu lililotengwa na Serikali, ujenzi unaotarajiwa kuanza Juni mwaka huu.
Akitoa mchanganuo wa athari za mafuriko hayo yaliyoikumba Kilosa wakati wa mkesha wa Sikukuu ya Mwaka Mpya Desemba 31 mwaka jana, Dendego alisema kaya 6,168 zenye watu 25,806 zimeathirika katika wilaya hiyo yenye wakazi 582,000.
Alisema mpaka sasa watu wapatao 9,000 wanaishi kwenye kambi nne tofauti za Mazulia, Kimamba, Kondoa na Chanzulu, zilizojengwa kwa mahema ambayo hata hivyo alisema hayawezi kuhimili mvua za masika zilizoanza kunyesha sasa, na zinazotarajiwa kufikia kikomo Mei mwaka huu.
"Tunahitaji zaidi vifaa vya ujenzi ili kuwajengea nyumba waathirika wakati huu wakiendelea kuhifadhiwa kwenye kambi zao... nyumba nyingi zimebomoka kutokana na mafuriko, na maeneo yaliyoathirika zaidi tumewazuia wananchi wasirejee.
"Wapo baadhi bado wanakaidi agizo la Serikali... wale waliogoma kuhama kwenye maeneo ya hatari yaliyoathirika, wataondolewa kwa nguvu na kupewa viwanja na vifaa vya ujenzi ili wajenge makazi mapya ya kudumu," alisema Dendego.
Akizungumzia waathirika 7,647 (wanaotoka kaya 1,600) walioko kwenye kambi ya Mazulia iliyopo katika kiwanda cha zamani za kutengeneza busati, Dendego alisema wamebaini kuwa watoto wengi kwenye kituo hicho hawajaandikishwa shule, hivyo wataanza mchakato wa kuondoa tatizo hilo.

You liked this post? Subscribe via RSS feed and get daily updates.

0 comments:

Post a Comment