Mgomo wa matatu watatiza usafiri!

Maelfu ya wakazi wa miji mikuu nchini Kenya wamekosa usafiri, kufuatia mgomo wa magari ya abiria maarufu kama matatu. Wengi walilazimika kutembea kutoka makwao hadi mijini na wengine kuamua kukaa nyumbani.
Wahudumu wa magari hayo ambayo yanategemewa na wakenya wengi wamedai kuwa wanahaingishwa na polisi. Wanasema polisi pia hudai hongo kutoka kwao.
Polisi hata hivyo wanashutumu wahudumu hao kwa kuvunja sheria za barabarani. Baadhi ya sheria hizo ni mpya, kama ile inayohusu viwango vinavyoruhusiwa vya kelele.
Mgomo wa leo pia umetatiza shughuli ya kufunguliwa shule kote nchini. Wengi wa wanafunzi na walimu hawakuweza kufika kutokana na mgomo huo.
Kwa muda sasa matatu zimekuwa zikilaumiwa kwa ukiukaji wa sheria ambao umechangia katika kuongezeka kwa ajali za barabarani. Polisi wamesema wataendelea kutekeleza sheria hadi wahudumu wa matatu wasalimu amri.

You liked this post? Subscribe via RSS feed and get daily updates.

0 comments:

Post a Comment