Wilaya ya Manyoni yajenga wodi ya watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano

Mama Salma kikwete akiwa amevaa vazi la kiasili la mkoa wa Dodoma
Na Anna Nkinda - Maelezo, Manyoni
17/11/2009 Jumla ya Tshs. 84,807,922/= zimetumika katika ujenzi wa wodi ya watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano katika Hospitali ya wilaya ya Manyoni iliyopo mkoani Singida.
Hayo yamesemwa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa wilaya hiyo Fotunata Malya wakati alisoma taarifa ya ujenzi wa wodi hiyo kwa Mke wa Rais Mama Salma Kikwete aliyekuwa na ziara ya kikazi ya siku moja wilayani humo.
Malya alisema kuwa ujenzi wa wodi hiyo ambao ulianza mwezi wa tisa mwaka 2007 na kukamilika mwezi wa tano mwaka huu umegharamiwa na Serikali kuu ambayo imetoa Tshs. 82,579,000/= pamoja na Halmashauri ya wilaya ambayo imetoa Tshs.2,228,300/=.
Alisema, "Ujenzi wa wodi hii ni matokeo ya kuongezeka kwa mahitaji ya mahali pa kulaza watoto kutokana na kuwepo kwa wodi ndogo isiyokuwa na nafasi ya kutosha. Msongamano huo ulifikia kiasi cha wagonjwa wawili au zaidi kulazwa katika kitanda kimoja".
Mkurugenzi huyo alisema kwamba wodi hiyo inakabiliwa na upungufu wa vitanda 40, magodoro 40, mashuka 240, vyandarua 80, mablanketi 80, makabati madogo ya ukutani 40, Oxygen Concentrator machine mbili, ENT set 10, Fumes/dust sucking machine moja na Resuscitation kit nne. Alizitaja gharama ya vifaa hivyo kuwa ni Tshs.25,678,000/=.
Akiongea na wananchi wa wilaya hiyo mara baada ya kufungua wodi hiyo Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema kuwa kujengwa kwa wodi hiyo kutaboresha huduma ya tiba kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano na hivyo kupunguza vifo vyao.
Ili kupunguza tatizo la vifo vya kina mama wajawazito na watoto Taasisi ya WAMA iliipatia Hospitali hiyo msaada wa vitanda vya kujifungulia viwili, Delivery kit moja, vitanda vya Hospitali vinne, magodoro manne,mashuka nane,chombo cha kusikilizia mapafu au mapigo ya moyo (Stethosope) moja na mashine ya kupimia ugonjwa wa moyo moja. Thamani ya vifaa vyote ni Tshs.3,239,800/=.
Wilaya ya Manyoni ina hospitali tatu moja ni ya serikali na mbili ni za mashirika ya dini ambazo ni St. Gaspar Itigi na Kilimatinde, vituo vya afya vinne vitatu vya serikali na kimoja ni cha shirika la dini na zahanati 48 kati ya hizo 38 ni za serikali na kumi ni za mashirika ya dini na watu binafsi.

You liked this post? Subscribe via RSS feed and get daily updates.

0 comments:

Post a Comment