16/11/2009 Serikali wilayani Bahi mkoani Dodoma imefanikiwa kuwarejesha shuleni wanafunzi watoro 594 kati ya wanafunzi1012 ambao waliacha masomo ya elimu ya msingi na sekondari na kujishughulisha na kazi mbalimbali za kijamii.
Hayo yamesemwa jana na Mkuu wa wilaya hiyo Betty Mkwasa wakati akisoma taarifa ya maendeleo ya wilaya kwa Mke wa Rais Mama Salma Kikwete aliyekuwa na ziara ya kikazi ya siku moja wilayani humo.
"Kwa upande wa shule za msingi kulikuwa na wanafunzi watoro 776 wavulana ni 364 na wasichana 412 wanafunzi waliorejeshwa ni 464 wavulana 201 na wasichana 263 na shule za sekondari kulikuwa na watoro 236 wavulana 107 na wasichana 129 waliorejeshwa ni 130 wavulana 74 na wasichana 56", alisema Mkwasa.
Mkuu huyo wa wilaya aliendelea kusema kuwa bado wanaendelea kuwafuatilia wanafunzi wengine waliobaki ili nao waweze kurejeshwa shuleni na kuendelea na masomo yao kwani wanafunzi waliorejeshwa katika shule za sekondari ni sawa na asilimia 55 na shule za msingi ni asilimia 59 tu.
Aliendelea kusema kuwa hivi sasa tatizo la utoro limepungua katika wilaya hiyo kutokana na kufungua shule za msingi mpya nane katika maeneo ya wafugaji yenye watu wengi, shule 23 za msingi zipo katika mpango lishe wa School Feeding Programme (WFP) , mashirika mbalimbali kupitia kanisa la Anglikana kutoa lishe kwa baadhi ya shule na utoaji wa semina na maelekezo ya mara kwa mara kwa walimu wakuu na waratibu elimu kata kuhusu mahudhurio ya lazima.
Kuhusiana na ulipaji wa madeni ya walimu wa wilaya hiyo Mkwasa alisema kuwa Serikali imewalipa walimu 290 Tshs. 112,762,653/= madai ya fedha za uhamisho, masomo, likizo, matibabu na posho ya kujikimu ambayo yaliyohakikiwa mwezi Februari mwaka huu na kulipwa mwezi wa kumi 2009.
Alizitaja changamoto mbalimbali za elimu wanazokabiliana nazo kuwa ni pamoja na upungufu wa walimu katika fani za masomo ya sayansi, upungufu wa vifaa vya kujifunza na kujifunzia, miundombinu hafifu katika maeneo ya kazi kama umeme, maji na barabara, upungufu wa majengo yakiwemo madarasa, mabweni, hosteli, vyoo, nyumba za walimu na majengo ya utawala.
Kwa upande wake Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) aliwataka wanafunzi wa wilaya hiyo kuachana na tabia ya utoro ambayo haitawasaidia kitu chochote katika maisha yao ya baadaye badala yake waende shule.
Mama Kikwete alisema, "ninachowasihi watoto wangu angalieni sana mazingira yasiwatawale bali ninyi ndiyo myatawale mazingira hakika kwa kufanya hivyo mtakuja kufanikiwa katika maisha yenu kwani kuna baadhi ya wanafunzi katika umri wenu wanatawaliwa na mazingira na kujiingiza katika makundi yasiyofaa na hivyo kuharibikiwa kimaisha".
Akiwa wilayani humo Mama Kikwete alitembelea shule ya watoto wenye ulemavu wa kusikia iliyopo Kigwe na kuona jinsi wanafunzi hao wanavyoishi na kusoma shuleni hapo pia aliwapatia zawadi ya Tshs. 500,000/= fedha ambazo watazitumia kununua jezi pamoja na mipira.
Wilaya ya Bahi inajumla ya madasara 68 ya elimu ya awali yenye wanafunzi 6358, shule za msingi 70 zenye wanafunzi 32156 wakiwemo wavulana 16178 na wasichana 15978 na shule za sekondari 20 zenye wanafunzi 3146 wasichana 1346 na wavulana 1800.
Taasisi ya WAMA ilivichangia vikundi vya wanawake wajasiriamali vilivyopo wilayani humo Tshs. 1,500,000/= fedha ambazo zitatumika kuinua mitaji ya vikundi hivyo.
Mwisho.





0 comments:
Post a Comment