Wanafunzi walemavu wa shule ya msingi Kizega wafanya vizuri katika mitihani yao ya darasa la saba!!

Mama Salma Kikwete akiongea na wananchi mkoani Singida
Na Anna Nkinda - Maelezo, Iramba
18/11/2009 Wanafunzi wenye ulemavu wamekuwa wakifanya vizuri katika mitihani yao ya Taifa baada ya wazazi wao kuona umuhimu wa kuwapeleka shule kwa wakati jambo ambalo limeifanya Serikali kuwapatiwa huduma mbalimbali wanazostahili kutokana na mahitaji yao.
Hayo yamesemwa jana na Mwalimu mkuu wa shule ya Msingi Kizega yenye kitengo cha wanafunzi wenye ulemavu Isaack Dagharo wakati mke wa Rais Mama Salma Kikwete alipotembelea shule hiyo kwa ajili ya kujionea maendeleo ya elimu wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku moja katika wilaya ya Iramba.
Mwalimu Dagharo alisema kuwa shule hiyo ina makundi matatu ya aina tatu za walemavu ambao ni walemavu wa macho (wasioona) 15, walemavu wa ngozi (albino) 18 na walemavu wa viungo wawili hivyo kuifanya idadi ya wanafunzi kuwa 35 kati ya hao wavulana ni 25 na wasichana ni 10.
Aliendelea kusema kuwa wanafunzi wote 10 walemavu waliofanya mitihani ya darasa la saba tangu mwaka 2006 hadi mwaka 2008 waliweza kufaulu mitihani yao na kujiunga katika shule za Sekondari Mpwapwa, Shinyanga, Kinambeu na shule ya sekondari ya wasichana ya Tabora .
"Kutokana na kutokuwa na shule maalum ya walemavu katika mkoa wa Singida wanafunzi hawa wanasoma na wanafunzi wasio walemavu kwa kuchanganyika madarasani lakini wanafunzi walemavu wao wanaishi katika baweni yaliyopo hapa shuleni", alisema Mwalimu Dagharo.
Shule hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na upungufu wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia hasa vitabu vya Braille kwa wasioona hii imesababishwa na mabadiliko ya mitaala ya mara kwa mara, kukosekana kwa maji safi na umeme, upungufu wa thamani katika bwalo la chakula hasa meza na viti.
Alisema, "Changamoto zingine ni kukosekana kwa usafiri wa gari, kukosekana kwa lotion maalum, kofia na miwani kwa wanafunzi wenye ulemavu wa ngozi kwa ajili ya kujikinga na jua pamoja na upungufu wa matundu ya vyoo".
Kwa upande wake Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleao (WAMA) aliwataka wanafunzi hao kusoma kwa bidii na kuendelea kufanya vizuri katika mitihani yao kwa kufanya hivyo matokeo yake watayaona hapo baadaye.
Shule hiyo ilianzishwa mwaka 1959 ikiwa ni shule ya wanafunzi wa kawaida lakini mwaka 1992 kitengo cha wanafunzi walemavu wasioona kilianzishwa kwa kuwaandikisha wanafunzi wanne tangu kuanzishwa kwake hadi sasa kitengo hicho kinawezeshwa na Halmashauri ya wilaya ya Iramba na wizara ya Elimu na mafunzo ya ufundi.
Taasisi ya WAMA pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo ya elimu waliichangia shule hiyo zaidi ya shilingi milioni tatu na laki tano ili ziweze kuwasaidia kununua mahitaji mbalimbali kwa ajili ya wanafunzi hao pia waliwapatia mafuta ya kupikia, mafuta ya taa, unga wa ngano, mchele, mahindi, maharage, sukari pamoja na chumvi.

You liked this post? Subscribe via RSS feed and get daily updates.

0 comments:

Post a Comment