Wanafunzi 220 wapata mimba kwa muda wa miezi kumi mkoani Kigoma!!

Na Anna Nkinda - Maelezzo, Kigoma
29/10/2009 Jumla ya wanafunzi 220 wa shule za Msingi na Sekondari Mkoani Kigoma wamepata ujauzito kuanzia mwezi wa kwanza hadi wa kumi mwaka huu na hivyo kushindwa kuendelea na masomo yao.
Hayo yamesemwa jana na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Kanali Mstaafu Joseph Simbakalia wakati akisoma taarifa ya maendeleo ya mkoa huo kwa Mke wa Rais Mama Salma Kikwete aliyepo mkoani humo kwa ziara ya kikazi ya siku mbili.
Taarifa ya Mkuu wa Mkoa huyo ilifafanua kuwa wanafunzi wa shule za Sekondari waliopata ujauzito ni 163 na wa shule za msingi ni 57.
Kwa upande wa mwaka jana wanafunzi waliopata ujauzito ni 167 ambapo wanafunzi wa shule za sekondari ni 85 na shule za Msingi ni 82.
Ili kukabiliana na tatizo hilo mkoa huo unajenga hosteli ambazo zitawasaidia wanafunzi wa kike kukaa shuleni wakati wote wa masomo na hivyo kuepukana na mazingira ambayo yatawafanya wapate mimba kirahisi.
Kwa upande wake Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alipata muda wa kuongea na wazazi pamoja na wanafunzi wa kike wa mkoa huo na kuwataka kutojiingiza katika mapenzi kabla ya wakati bali wasubiri hadi pale watakapomaliza masomo yao.
"Hao wanaume wanawadanganya tu, wanawachezea miili yenu na hawawapi kitu chochote zaidi ya ujauzito na ugonjwa wa UKIMWI. Elimu ni mkombozi wa maisha yenu hivyo basi shirikianeni katika masomo ili muweze kufaulu vizuri na kujiunga na vyuo vikuu", alisema Mama Kikwete.
Alisema, "Mkumbuke kuwa jukumu la ulezi wa mtoto ni la jamii nzima si la mzazi peke yake kwani kuharibika kwa mtoto wako ni kuharibika kwa taifa zima hivyo basi sote kama wazazi tunajukumu la kupunguza kasi ya upatikanaji wa mimba za utotoni kwa watoto wetu na kuhakikisha kuwa watoto wanakuwa katika maadili mema ya kitanzania".
Mkoa huo unajumla ya shule za msingi 621 kati ya mahitaji 668 hivyo kuna upungufu wa shule 46 na shule za sekondari 130.

You liked this post? Subscribe via RSS feed and get daily updates.

1 comments:

  1. Kwa kweli swala hili ni ngumu sana na inabidi tulifanyie kazi bila hivyo taifa lote la kesho litakuwa halina elimu.

Post a Comment