UZINDUZI WA KIPINDI CHA TELEVISHENI CHA MAYROSE TALK SHOW!!

Mayrose Kavura Majinge
Shirika la Wadhamini la Huduma za Maendeleo ya Jamii (RTCDS) linawaarifu kuwa tarehe 9 Oktoba,2009 siku ya Ijumaa kutakuwa na Uzinduzi wa kipindi cha Mayrose TV Talk Show katika viwanja vya Sabasaba Ukumbi wa PTA kuanzia saa 7.30 mchana hadi saa 11jioni.
Madhumuni ya kipindi cha Mayrose Talk Show ni kutoa elimu juu ya mambo ya kijamii, maisha ya kila siku na maendeleo kwa ujumla. Kipindi kinalenga zaidi mtu mmoja mmoja kwa minajili ya kuwasaidia vijana waweze kukabiliana na umasikini.
Mada itakayojadiliwa siku ya uzinduzi inasema:- “ Ni vipi mtu anaweza kupata elimu bora?”

Watu mbalimbali mashuhuri wameshiriki katika maandalizi ya kipindi chetu kwa kutoa mawazo yao. Baadhi yao ni Prof. Palamagamba J. Kabudi (Kiuweledi ni Mwanahabari na Mwanasheria pia ni Mhadhiri Chuo Kikuu cha Dar es salaam); Ndg. Ibony Moalim ( Meneja Uchapishaji Blackmark Corporations); Ndg. Guido Msita( Mkurugenzi Mtendaji Blackmark Corporations); Dr. Adolf Mihanjo (Mwanafalsafa na Mhadhiri Chuo Kikuu cha Dar es salaam); Ndg. Isaac Mruma; Ndg. Damas Mfugale ( Mkurugenzi Mtendaji- Peacock Hotels); Eng. Edward Ngowi; Ndg. Protas Mwageni; Ndg. Ongito Hodari ( Mkuu wa Maktaba Chuo cha Usimamizi wa Fedha) Dr. Ali Mcharazo ( Mkuu wa Maktaba Tanzania); Kanali Mstaafu Idd Kipingu; Ndg. Ghonche Materego ( Katibu Mtendaji Baraza la Sanaa la Taifa); Aliyekuwa Kaimu Mufti Hayati Sheikh Suleimani Gorogosi; Askofu Methodius Kilaini; Mwl. Charles Shilindi (Mkuu St. Emmanuel High School );Ndg. Geofrey Tengeneza (Afisa Uhusiano Mwandamizi – Bodi ya Utalii); Ndg. Emmanuel Likuda (Mratibu Entertainment Masters). Ni wengi sana tuliowashirikisha siwezi kuwataja wote..

Siku ya uzinduzi tutakuwa na baadhi yao, pamoja na wengine watakaokuwepo ni Ndg. Eric Shigongo (Mjasiriamali maarufu na mmiliki wa vyombo vya habari vya Global Publications); Ndg. Mrisho Mpoto ( Msanii maarufu) na wengine wengi kutoka Vyuoni, shule mbalimbali, mashirika yasiyo ya kiserikali na mashirika ya umma pamoja na watu mbalimbali.

Elimu ni ufunguo wa maisha, bila elimu maisha hayaendi vizuri. Tunahitaji elimu bora ili tuweze kujikwamua na Umasikini tulionao Watanzania.
Hata vitabu vitakatifu vinaeleza umuhmu wa elimu kwa wanadamu. Kwa mfano tukiangalia katika Biblia Takatifu kwenye kitabu cha Mithali ya Sulemani kimesisitiza umuhimu wa elimu huku kikisema elimu ni Uzima wa mtu…
Vile vile katika Quran Tukufu katika Surrat Iqraa Bismirabika imeeleza juu ya elimu.
Kwa mantiki hiyo tunasisitiza wengi mfike kupata elimu itakayotolewa siku ya Ijumaa tarehe tisa pale PTA Sabasaba. Inawezekana wengine wakasema mbona PTA ni mbali na makazi yao? Naomba wakumbuke maneno matakatifu juu ya elimu. Hasa ndani ya quran tukufu imeeleza bayana kuwa: “Uifuate elimu hata mpaka Uchina”
Mada itakayojadiliwa ni muhimu sana hakikisha umeshiriki kwa kufika
Kwa kuzingatia mchango wa Baba wa Taifa tumeamua kuzindua kipindi katika mwezi huu wa Oktoba ambao ni wa kumbukumbu ya Kifo cha Baba wa Taifa.
Suala la elimu bora limepewa kipau mbele kwa kuzindua kipindi hiki kwani kwa kutumia Elimu Bora tutaweza kupambana na Adui watatu ambao waliainishwa na hayati Baba wa Taifa (Umasikini, Maradhi na Ujinga). Katika kumuenzi Mwl. Julius K. Nyerere tunaalikwa wote kushiriki mada hii kwa kufika ukumbi wa PTA viwanja vya sabasaba na kwa walio nje ya Dar es salaam waangalie Star Tv kuanzia saa 9 alasiri siku hiyo na wachangie mada kwa kupiga simu namba itakayotolewa siku hiyo..
.
Ndugu Watanzania wenzangu, tukijua namna ya kupata elimu bora tutakuwa tumepata njia mbadala ya kufikia mipango ya maendeleo yetu.
Pamoja na Mada ya Elimu Bora itakayotolewa siku ya uzinduzi kutakuwa na burudani mbalimbali. Hakuna Kiingilio. Kipindi kitarushwa moja kwa moja kupitia Star TV. Tunaomba watu wafike kwa muda uliopangwa.

Baada ya siku ya uzinduzi kipindi cha Mayrose Tv Talk Show kitaendelea kuonekana Star Tv kila siku ya Jumapili saa 8 hadi saa 9 mchana. Fuatilia ili upate ufumbuzi wa mambo mbalimbali juu ya maisha . Mada zitakazofuata baada ya Elimu Bora ni pamoja na;-
Namna gani utaweza kutambua kipaji chako na kukifanya kikupe faida
Ni vipi utapata ajira
Ni vipi utapata nguvu na uwezo wa kupata unachotamani?
Nidhamu inachangia vipi maendeleo yako?
Ufanye nini ili uheshimike?
Imani inasaidia vipi kuleta maendeleo yako?
Ni vipi watanzania tutaweza kujiamini na kujitegemea.
Hizi ndizo mada za awali zilizoandaliwa kwa uchunguzi wa kina ili kumkomboa Mtanzania. Mada zingine zitaandaliwa kulingana na mahitaji ya wafuatiliaji wa kipindi chetu
Kwa namna ya pekee tunawashukuru wadhamini wa uzinduzi huu ambao ni Vayle Springs; Sayona Drinks; iPrint; Delfina Promotions Limited; na Star Tv kwa kukubali kurusha kipindi chetu. Tunatarajia wadhamini zaidi kwani kipindi hiki ni cha kila wiki.

Pamoja na kipindi hiki cha kila wiki Shirika la Huduma za Maendeleo ya Jamii linatoa Ushauri kuhusu mambo mbalimbali yanayokwamisha maendeleo. Kwa lolote unaloona ni kikwazo kwako njoo upate maelekezo ili ufikie malengo yako.
Huduma ya ushauri inatolewa kila siku ya Jumatatu na Ijumaa katika Ofisi zetu zilizopo Sido Makao Makuu Upanga – Inapakana na Shule ya Sekondari Aghakan Mzizima.

Wote mnakaribishwa.
Mayrose Kavura Majinge
Mwenyekiti Mtendaji,
The Registered Trustees of The Community Development Services.
P.O Box 7878,Dar es salaam
Email: mayrosedtalk@yahoo.com
Mob: 0655 376320/ 0754376320

You liked this post? Subscribe via RSS feed and get daily updates.

0 comments:

Post a Comment